Namungo wamtaka golikipa wa Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 05:46 PM Jul 03 2025
news
Picha Mtandao
kipa namba mbili wa Simba, Ally Salim

Baada ya kuachana na golikipa wao, Beno Kakolanya, klabu ya Namungo wameanza mazungumzo na kipa namba mbili wa Simba, Ally Salim ili kwenda kuchukua nafasi yake.

Inaelezwa mazungumzo ya pande hizo mbili yanaenda vizuri na wakati wowote dili hilo linaweza kukamilika.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema wameamua kutua kwa Salim kutokana na uwezo wake aliouonyesha akiwa na kikosi cha Simba, licha ya kwamba hapati nafasi mara kwa mara ya kukaa langoni.

“Mambo yakienda vizuri anaweza kuwa kipa wetu namba moja msimu ujao, ni kijana mzuri, ana uwezo, tumeona misimu miwili nyuma alipopewa nafasi baada ya Aishi Manula kuumia, alidaka michezo mikubwa ya Ligi Kuu, ikiwemo dhidi ya Yanga, mara mbili akiiwezesha Simba kushinda mechi ya Ligi Kuu na Kombe la FA.
“Pia Lig#i ya Mabingwa Afrika, nakumbuka mechi dhidi ya Wydad Casablanca, nyumbani na ugenini, kusema kweli ni kwa vile hapati nafasi tu ya kucheza mara kwa mara, akija kwetu atatusaidia na yeye atadhihirisha ubora wake,” alisema mmoja wa viongozi wa Namungo.

Inawezekana kuwa rahisi zaidi kwa Namungo kumpata kipa huyo aliyeanzia soka lake kwenye timu ya vijana ya Simba, kwani klabu Msimbazi iko mbioni kumsajili kipa wa JKT Tanzania, Yacoub Suleiman kwenda kusaidiana na Moussa Camara.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda, amewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa msimu ujao hawatorudi kinyonge.

Alisema kilichowatokea msimu uliomalizika siyo bahati mbaya, badala yake amesema kinachotakiwa sasa ni kusajili timu bora na yenye ushindani msimu ujao.

“Uzuri ni kwamba tume pambana na hatukushuka daraja, tumejifunza na tutajiandaa kuhakikisha tunakuwa timu shindani kwa kufanya maboresho maeneo mengi ambayo hatukuwa vizuri, ili uwe bora na mshindani unatakiwa kuwa na wachezaji wenye uchu na mafanikio, kikosi chetu kilikuwa na mapungufu maeneo mengi,” alisema Mgunda.

Timu hiyo imemaliza ikishika nafasi ya tisa, ikiwa na pointi 35.