Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China wanaofanya shughuli zao nchini, imeingia makubaliano ya kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 2,000 wa Kitanzania, ikiwa ni juhudi za kutatua changamoto ya ajira nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa ushirikiano huo unalenga kuwawezesha vijana kufahamu aina ya ajira zilizopo kupitia kampuni mbalimbali za Kichina zinazofanya kazi nchini Tanzania.
"Kwanza kabisa, kijana anapaswa kufahamu aina ya ajira zilizopo na kuweza kuchangamkia nafasi hizo kupitia makampuni yaliyo tayari kuajiri. Lengo kuu ni kupunguza changamoto ya ajira na kuwawezesha vijana wetu," amesema Ridhiwani Kikwete.
Aliongeza kuwa Wizara inasisitiza ushiriki wa vijana kwa wingi ili kunufaika na nafasi hizo, ambapo baadhi ya mchakato wa mahojiano (interviews) utafanyika moja kwa moja chuoni, hasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kampuni za Kichina yanayoshiriki katika mpango huu yanajumuisha yale yanayojihusisha na sekta za kilimo, uzalishaji wa maji, na nyinginezo, yakiwa na lengo la kutoa nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania zaidi ya 2,000.
"Tunashukuru Serikali ya China pamoja na Balozi wa China kwa ushirikiano huu wa kipekee unaosaidia kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wetu," amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania, Juma Sharobaro, alisema zaidi ya kampuni 100 kutoka China zimeshajiandaa kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania, kwa idadi inayokadiriwa kufikia kati ya 1,000 hadi 2,000.
"Ili kijana aajiriwe, anapaswa kutembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuonana na wawakilishi wa kampuni zinazoshiriki, ambapo atapata fursa ya kuzungumza nao na kuelewa aina ya kazi wanazotoa," amesema Sharobaro.
Mpango huu ni sehemu ya mikakati endelevu ya serikali kushirikiana na sekta binafsi za ndani na nje ya nchi katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED