NI zaidi ya upendo usiokadirika, mzazi kuhimili kumkumbatia mtoto mchanga saa nane hadi 24 mfululizo. Kibinadamu, siyo jambo rahisi kutimiza wajibu huo!
Katika Kanda ya Ziwa, hasa mkoani Mwanza, linatajwa kutawala, watoto wengi wanazaliwa njiti, wakiachwa pagumu wazazi, wauguzi na wadau.
Hao nao wanatoa kilio chao serikalini, kudai utafiti unaobaini chanzo cha kasi ya tatizo hilo.
Ni mada inayomvutia mwandishi wa Nipashe, akapanda ngazi kuelekea ghorofa ya tano la jengo jipya la ‘Mama na Mtoto’ katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure.
Ni jengo jipya lililoigharimu serikali Sh. Billioni 13 mahususi kutetea afya ya mama na mwanawe, kupunguza vifo vyao.
Baada ya kufika, anapokewa na kibao kinachomwelekeza iliko wodi ya watoto wachanga, penye huduma tajwa.
Anakutana na kitengo kwa jina ‘Infectious Baby’ penye huduma ya Watoto Wachanga Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (NICU).
Taratibu mhusika anasogelea penye maandishi ya Huduma ya Watoto Njiti (KMC), akihitaji kujua mengi kutoka kwa wahusika.
Ilikuwa wakati kalenda inasomeka Mei 15, ambayo kitaifa na kimataifa inatambulisha Siku ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Kangaroo au “Care Awareness Day’ (Watoto Njiti),
Mwandishi anakutana na Dk. Magreth Guranywa, Mkuu wa Idara ya Watoto hospitalini hapo, anayeeleza wimbi kubwa la watoto njiti kimkoa, akitumia mfano kila mwezi wanawapokea 150 hadi 200 wenye matatizo, bila kuwagawa kimakundi.
Anafafanua, mara baada ya kuwagawa wanaozaliwa kabla ya wiki wako 37; wenye viungo havijakamilika (njiti) wastani kati ya 70 hadi 90.
Dk. Magreth anaeleza idadi hiyo ni kubwa na maswali kwao wataalamu yanajengeka, kuhoji chanzo kuongezeka hali hiyo.
Hilo linafanyika, huku kukielezwa kuna hatua za kuchukuliwa historia za wazazi hao baada ya kujifungua, ili kutambua mzizi wa mkasa husika.
Inatajwa kiafya inaweza kugusa hali kama maradhi mbalimbali, zikiwamo presha au maambukizi wakati wa ujauzito.
Dk. Magrerth anaeleza shauku yake ni kuona utafiti unafanyika kuangalia tatizo husika na hatua za haraka zinachukuliwa, kupunguza.
Anaelimisha vya kuepuka kiafya vinajumuisha wajawazito kuhudhuria kliniki mapema, kwa sababu ndiko wanakoweza kubaini vyema dalili, viashiria au vidokezo hatari kwa mwanamke.
Mtaalamu huyo anasisitiza kuwa kliniki ni sehemu muhimu panakotegemewa na umma, kuhudumia na kutoa elimu ya vidokezo hatari kwa mjamzito.
Vilevile anasema, panakotambua dalili hatari ni kama vile mtoto kutocheza, kutokwa damu au ishara nyingine za kujifungua.
“Naiomba serikali na wadau waendelee kuangalia suala hilo kwa jicho la kipekee katika kuwasaidia kinamama hawa.
“Pia, utafiti ufanyike kupata chanzo hasa kusaidia kuzuia tatizo hili,” anaeleza na kuendelea:
“Sasa hivi hospitali inaendelea kupambana kuwatunza kuwahudumia na kuwatibu watoto hao kwa sababu ni moja ya idadi kubwa ya watoto wanaopokelewa hospital hapa”
SIRI YA MLIPUKO
Muuguzi Kiongozi wa Kitengo cha Watoto Wachanga hospitalini hapo, Chiku Mabuba, anasema wao ndio wanawapokea wanaozaliwa kabla ya muda na wenye uzito mdogo.
Chiku anasema kumekuwapo ongezeko kubwa la watoto hao, baada ya kuhamia jengo jipya la ‘Mama na Mtoto’.
Anaeleza awali kwenye jengo la zamani walipokea watoto 40 kwa mwezi, lakini mwaka 2022 walipohamia jengo jipya, idadi ikaongezeka maradufu.
Muuguzi Kiongozi huyo anataja kati ya mwaka jana hadi sasa, idadi imepaa kufika watoto 70 hadi 90 kila mwezi.
Hapo Chiku anaeleza: “Kuna wakati mama zao tunakaa nao, lakini wakionyesha wazi kukata tamaa wakati mwingine kuchoka kabisa.
“Hivyo, tukiwa sisi kama wauguzi tunawajibika kutoa elimu kwao hasa jinsi ya kuwahudumia watoto hao ikiwamo suala la usafi, lishe na namna ya kuwanyonyesha...”
Pia, anfafanua ni darasa linalomgusa mama anavyopaswa kumhudumia mtoto wake, hasa anapokuwa ‘amemfunga kangaroo.’
Anaeleza kuna kipindi wanakaa na kinamama, kati ya wiki hadi mwezi mzima, akisema mazingira ya wazazi hao kukaa hospitalini muda mrefu yanawachosha na kuwakatisha tamaa. Hivyo anasema, wanaendelea kutoa elimu kwa wahusika wasikate tamaa.
Kaimu Muuguzi Kiongozi kutoka hospitalini hapo, Paschal John, anasisitiza umuhimu wa mbinu iitwayo ‘kangaroo mother care’ kuwafikia wanaume kubeba mtoto kama ilivyo kwa mwanamke.
Anataja lengo la kufanikisha mguso wa ngozi kati ya mtoto na mzazi, ni kumpumguzia mzazi changamoto,
Pia, anasisitiza umuhimu wa usafi mtoto na mlezi, kuweka mbali uwezekano wa mtoto kuambukizwa.
Anatoa rai kwa wadau wataalamu kuendeleza utafiti wa kugundua chanzo cha ongezeko hilo, kupata majibu ya kudhibiti kinachojiri hospitalini hapo.
KINACHOENDELEA BUGANDO
Dismas Mauki, Muuguzi Kiongozi wa Kitengo cha Watoto katika Hospitali ya Rufani Bugando, jijini Mwanza anaungana kukiri kinachoongelewa na wenzake wa Hospitali ya Sekou Toure.
Anaeleza uzoefu wao Bugando, kwamba nyuma walivuka siku moja au mbili pasipo kupokea mtoto njiti na waliootokea waliangukia wastani mtoto mmoja.
Muuguzi huyo anataja hali imegeuka, hakuna siku inapita hawajapokea mtoto njiti, wakitoka Kanda ya Ziwa, ila mkoani Mwanza kunaongoza, akitaja idadi kati ya 30 hadi 40 kwa mwezi.
Kiafya anafafanua huwa wana uzito wastani gramu 800 hadi kilo 1.1 (gramu 1,100) wanaoanzua kuhudumiwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).
Anaeleza uzito wao unafika wastani wa kilo 1.3 (gramu 1300) hadi 1. 4 (gramu 1.400) ndio wanahamaishiwa eneo lao liitwalo Kangaroo, wakiweka kifuani kupata joto la mama.
Mtaalamu huyo wa Bugando anaungana na wenzake wa Sekou Toure, kudai utafiti ufanyike kujua mzizi wa mlipuko huo wa ugonjwa na haja ya mama kuhudhuria kliniki mapema.
Anasema ni hali inayomuandaa mjamzito akijifungua mtoto dhaifu kiafya, kunakuwapo maandalizi yanayojitosheleza hospitalini kumhudumia mzazi na mtoto.
Hapo ana mfano, mtoto njiti anayezaliwa katika zahanati, mpaka afike penye sahihi, anakuwa amepoteza joto jingi na kumhatarishia afya yake.
“Mpaka wamtoe huko watakuwa wameshachelewa, lakini mama huyo akiwahishwa na kujifungulia katika mazingira mazuri uwezekano wa kumsaidia mtoto huyo kwa muda mfupi upo na akaendelea vizuri zaidi,” anaeleza.
Akataja mafanikio ya upendo ya kwa mzazi wanaombeba mtoto.
WADAU NA WAZAZI
Ezra Shemayo, Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa asasi Babymoon Africa, anaiambia Nipashe umuhimu wa kangaroo kwa mzazi dhidi ya mtoto njiti.
Anaeleza hilo kufanyika kwa muda mrefu, ikiwezekana saa 24 kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Ezra anaeleza upande wa pili, kuna ugumu wa mzazi kutenda kwa saa 24, wao asasi ya Babymoon wameliinglia kati kuwasaidia wazazi wa njiti,
Anataja wanawapa ‘vibebeo’ kumsaidia mama, baba au mlezi mwingine kuondokana na matumizi ya nyenzo kama kanga na taulo vinavyoweza kufunguka.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii na wazazi waliopata watoto njiti wachukulie kama tatizo la kawaida, kama yalivyo magonjwa mengine,” anasema.
Pia, Mkurugenzi - Ezra, ana nasaha kuwa ‘vibebeo’ vina mchango kupunguza vifo vya watoto na vinawaongezea watoto joto, upendo na kuwahudumia muda mrefu
Albeny James, Mkurugenzi wa asasi Babymoon Afrika, anataja utayari wao kushirikiana na serikali ama kutafiti kubaini kilicho nyuma ya pazia, kuhusu kuongezeka watoto njiti kwa Kanda wa Ziwa.
Mzazi Rosemary Kusekwa anaeleza uzoefu wake kulea mtoto njiti kwamba kiafya alianza kuonyesha dalili mbaya, kabla hajaanza kuhudhuria kliniki na alipofanyiwa kipimo ‘Ultra Sound’ akabainika kupungukiwa maji mwilini.
Anasimulia ikawa changamoto kwa mtoto na akashauriwa kubaki hospitalini akiangaliwa, alikodumu wiki moja.
Akarejea nyumbani na baada ya siku mbili anasema, hali yake ikawa tofauti, akihisi tumbo sehemu ya chini inauma sana ndipo akakimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa Sekou Toure, alikoelezwa na matabibu ‘njia imefunguka na mtoto yupo tayari kutoka.’
“Ndio ikawa hivyo, nikajaliwa kujifungua mtoto njiti akiwa na umri wa miezi sita na wiki mbili sasa hivi ana miezi sita na wiki tatu.
“Ukweli, kulea mtoto njiti ni changamoto kubwa, kwa sababu ni kitu unakutana nacho kigeni na mtoto huyo anahitaji uangalizi mkubwa, ikiwamo umakini kumpatia dawa anazozitumia.
“Pia unyonyeshaji kila baada ya masaa matatu, mtoto anatakiwa kupata maziwa ambayo nayo ni kwa kipimo elekezi,”anaeleza mzazi huyo
Vilevile, Lusia John, aliyekuwa na muda wa siku sita tangu ajifungue, anaunga mkono hoja ya ‘uangalizi wa mtoto huyo ni muhimu kuliko chochote’ na hatari endapo maelekezo ya kumhudumia yanapokosewa.
Pia, anashukuru kuwa mnufaika wa ‘kibebeo’ anachokieleza kuwa msaada unaomrahisishia kumbeba mtoto, kwani kabla mwanzoni alisubiri msaada wa kufungwa kanga.
Kwa sasa anasema, anaweza kujifunga mwenyewe na mtoto anakaa sawa, kuliko matumizi ua kanga na taulo.
William Isack, mzazi wa kiume wa mtoto aliyezaliwa njiti, ambaye kwa sasa yupo kidato cha kwanza anasimulia walivyopita wakati mgumu kumlea mtoto wao.
Ananena: “Kinababa tusiwaachie mzigo wake zetu peke yao, pale wanapopata nafasi wasaidie kwa sababu mtoto ni wenu nyote.”
Hayo yanajiri huku Ripoti za WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), pamoja na PMNCH, inataja ushirikiani huo unaangazia afya ya mama, watoto, vijana.
Kuhusu wanaozaliwa kabla ya wakati, makadirio ya wasimamizi afya yanaonyesha mwaka 2020, takriban watoto milioni 13.4 walizaliwa njiti, huku wastani milioni moja wamefariki.
Pia, hali hiyo zaidi inatajwa kutokea Ukanda wa Jangwa la Sahara na Asia ya Kusini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED