HADI sasa katika maeneo mengi nchini yanayopakana na mbuga za wanyama na mapori ya akiba, kama vile Hifadhi ya Taifa za Mikumi, Ruaha, Katavi, Serengeti, na Selous (Nyerere National Park), wakazi wake wameendelea kukumbwa na changamoto za uvamizi wa tembo kwenye mashamba yao.
Tembo wakiwa miongoni mwa wanyama wakubwa na wenye nguvu, hushambulia mazao ya wakulima, hata kusababisha hasara kubwa kiuchumi, uhaba wa chakula na wakati mwingine migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Katika namna ya kukabili shida hizo, inatajwa kuna mbinu za kitaalamu zenye ufanisi kuwazuia tembo wavamizi mashambani, lakini wakulima wengi hushindwa kuzimudu kutokana na gharama zake kubwa.
Mbinu hizo zinatajwa na wataalamu zinajumuisha kuwekwa uzio wa umeme ambao ni ghali kuzisimamisha kwa mkulima mmoja mmoja, huku zinahitaji matengenezo ya kila mara.
Hapo hutumia vifaa vya kielektroniki vinavyotoa sauti na mwanga kuwachanganya tembo, pia utumiaji ndege zisizo na rubani, maarufu ‘drones’ zinazoweza kuwatambua na kuwafukuza.
Shida kuu ni gharama kubwa za kuzinunua, pia uendeshaji wake ni mgumu kwa wakulima wa kawaida.
Mbadala wake, wakulima wamekuwa wakibuni mbinu za asili, pia kisasa kuwafukuza tembo na kulinda mashamba yao. Hapo zipo kadhaa.
KILIMO CHA PILIPILI
Wakulima huwa wanatengeneza uzio wa pilipili kali zinazopandwa pembezoni mwa mashamba au kutumika mchanganyiko wa pilipili na mafuta ya taa, kutengeneza ‘bomu la pilipili.’
Vilevile, inatajwa kuwapo tofali la pilipili na wakati mwingine pilipili kavu huchomwa moto na harufu kali itakayo hapo, huwachukiza tembo hata wakayaepuka maeneo hayo.
Hapo kuna ufafanuzi wa mkulima Juma Mohamed, kutoka kijiji cha Msongozi wilayani Mvomero, ambako kumepakana na Hifadhi ya taifa ya Mikumi mkoani Morogoro.
Juma ni miongoni mwa wakulima wenye mafanikio makubwa kwa kutumia mbinu ya kilimo cha pilipili kukabiliana na tembo wavamizi shambani.
“Awali tulikuwa hatupati mavuno kabisa. Tembo walikuwa wanavamia mashamba kila msimu na kutumalizia kila kitu,” anatamka na anaendelea:
“Lakini, tangu tuanze kutumia pilipili – kama vile kupanda pilipili pembezoni mwa mashamba, kutengeneza tofali la pilipili, kuchoma pilipili kavu na hata kutumia mchanganyiko wa pilipili na mafuta ya taa, hali imeanza kubadilika.
“Harufu kali ya pilipili inawachukiza tembo. Ingawa si kwamba wameacha kabisa kuja, lakini wamepungua sana! Kwa sasa, angalau tunapata sehemu ya mavuno yetu.”
Mkulima Juma anasimulia kwamba, suala la kuwa mbali na kuwafukuza tembo, kuwa ni mageuzi katika kilimo cha pilipili kinachokuwa chanzo cha kipato kwa familia yake, kwani sehemu ya mazao hayo anaziuza sokoni.
Anaendeleza simulizi akinena: “Ni faida mbili kwa moja. Tunajilinda na tembo, pia tunapata pesa. Tunafundishana kijijini mbinu hizi, kwa sababu tumegundua zinafaa sana,”
Ni ushuhuda unaofafanua namna mbinu ya kutumia pilipili unakabili athari za tembo shambani, kwa jamii zinazokumbwa na migogoro ya tembo wa hifahini na kazi wakulima shambani.
UFUGAJI NYUKI
Mkulima anayejitambulisa kwa jina la Yamungu kutoka kijiji cha Mkata, mkoani Pwani, anasimulia namna tembo wanawaogopa nyuki, kutokana na maumivu wanayoyapata wakidungwa, hasa masikioni na mkiani.
Hilo anasema, limewafanikisha wakulima kuwazuia waingie katika mashamba yao. Pia, ni mbinu anayoitaja kuwapatia asali, hata kuwa chanzo mbadala cha kipato kwao.
Mkulima Yamungu kutoka kijijini Mkata, anajitambulisha kuwa miongoni mwa wanaotumia silaha ya nyuki, kukabaliana na adui tembo shambani kwao.
Anasimulia: “Tembo huwaogopa sana nyuki hasa wanapodungwa kwenye maeneo nyeti kama vile masikio na mkiani.
“Tangu tuanze kuweka mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba yetu, tembo wamekuwa wakikwepa kabisa mashamba haya. Wakitikisika kidogo tu, nyuki huanza kuwashambulia na wao hukimbia haraka sana.”
Anaendelea kufafanua njia mbadala wanaotumia, akisema “mbinu hii ya uzio wa mizinga ya nyuki haijasaidia tu kupunguza migogoro kati ya tembo na wakulima, pia imekuwa na manufaa ya kiuchumi.”
“Mbali na kuzuia tembo, tunapata asali nzuri sana ambayo tunaiuza na kupata kipato cha ziada.
“Sasa mashamba yetu ni salama zaidi na familia yangu inanufaika mara mbili, chakula na biashara ya asali,” anaongeza mkulima Yamungu.
Mbinu za ufugaji nyuki zinatajwa kutambulika kuwa rafiki na zenye mazingira endelevu katika kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori, hususan katika maeneo jirani na hifadhi na mapori ya akiba nchini.
KELELE, MIALIKO KIJIJINI
Hizo zinatajwa kuwa silaha nyinginezi zinazotumika kwa wakulima, kupitia mbinu ya upigaji kelele kwa nyenzo kama ‘vuvuzela’, mapipa au vyuma, inayowaogopesha tembo hata wanakimbia kuhama eneo husika.
Aidha, inafafanuliwa na wataalamu hao kuwa baadhi ya vikundi vijijini vimeanzisha doria za kijamii, vikitoa taarifa, pindi tembo wanapoonekana wakielekea mashambani.
Hao hujitokeza haraka kuwafukuza wanyama hao, wakati huohuo serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ina program maalumu ya kusomesha vijana watakaosaidia kuwafukuza tembo wanaonekana kwenye maeneo yenye athari.
MWANGAZA WA NJE
Taa za mwangaza wa nje katika baadhi ya maeneo, inatajwa na wakulima kwamba wameanza kuzitumia. Imo jua inayowaka na kuzimika usiku, ili kuwatisha tembo.
Wanyama hao, huchukulia mwanga kuwa unaobadilika kuwa ishara ya hatari katika maeneo hayo husika.
Mkulima kwa jina moja, Mariam kutoka kijiji cha Doma, mtaa wa Kibalawala, ni miongoni mwa waliopata nafuu kutokana na matumizi ya taa za sola, unaowaka na kuzimika kwa zamu (katika kuzuia tembo kuvamia mashamba yao.
Mariam anaisimulia Nipashe akisema: “Tulikuwa tunaamka usiku kwa hofu kubwa, tukihofia tembo kuingia mashambani. Lakini, tangu tuanze kutumia taa hizi za sola zinazowaka na kuzimika kwa zamu, tumepata ahueni.
“Tembo huwa hawapendi mwanga unaobadilika-badilika, wanadhani kuna hatari, hivyo huamua kugeuka na kurudi walikotoka.”
Ingawa si suluhisho la kudumu kwa kila mkulima, Mariam anasema kwa upande wake anaitaja “njia hii imesaidia kupunguza uvamizi wa tembo kwa kiasi kikubwa.”
Anaifafanua kwa kauli: “Hawajaacha kabisa kuja, lakini mara nyingi wakiona mwanga huo hubadilisha mwelekeo.”
“Imetusaidia sana hasa msimu wa mazao unapokaribia kuvunwa. Kwa kweli, hata usingizi umerejea nyumbani,” anajigamba, katika hulka inayoambatana na tabasamu.
VIBANDA VIREFU MASHAMBANI
Pia, kunatajwa kuwapo mbinu mbadala wa kujenga vibanda virefu mashambani, wakulima wanakohamia, ikiwa sehemu ya jitihada zao kulinda mazao dhidi ya uvamizi wa tembo.
Katika hilo, baadhi ya wakulima katika maeneo yanayopakana na hifadhi na mapori ya akiba nchini wameamua kujenga vibanda mashambani wanakohamia, katika msimu mazao yanapoiva au kukomaa.
Bwakila Hamsini kutoka kijiji cha Doma, mtaa wa Kiondo mkoani Morogoro, naye ana maelezo yake kuwa:
“Baada ya kuona kuwa tembo wanavamia mashamba yetu hasa usiku, tuliamua kujenga vibanda shambani ili tuwe karibu na mazao.
“Hii inatusaidia kuwahi kuchukua hatua haraka, kabla ya tembo kuharibu kila kitu. Kwa mfano, tukisikia makelele au dalili yoyote ya tembo, tunapiga kelele, taa, au hata kuwasha moto mdogo ili kuwafukuza.”
Wakulima wanaoishi katika vibanda hivyo, pia wana mbinu mbadala kama kukinga mashamba kwa uzio wa pilipili, kupiga kelele na kueneza mwanga kukabilia wanyama, wakikiri ikichangia ufanisi.
Hata hivyo wanakiri: “Si maisha rahisi hasa kwa wanawake na watoto, lakini ni bora kuliko kupoteza kila kitu msimu wa mavuno.
“Tumejifunza kuishi mashambani kwa muda na tumejipanga kwa zamu kulinda,” anasema mkulima Yohana, kutoka kijiji jirani cha Mtakenini.
Hata hivyo, wakulima wanasema wanahitaji msaada zaidi kutoka serikalini na mashirika ya uhifadhi, kupata vifaa vya ulinzi, mafunzo na teknolojia rafiki kwa mazingira, ili kuimarisha ulinzi wa mashamba yao.
Mkulima Yohana anachokiri ni kwamba mbinu ya kuhamia shambani imekuwa suluhisho la muda kwa baadhi ya wakulima, akitaja kuwapo changamoto za usalama na ustawi familia, hasa kwa wanawake na watoto.
Ni jambo analolieleza kuonyesha umuhimu wa kutafutwa mbinu endelevu na rafiki kwa binadamu na wanyama katika kupunguza migogoro baina yao, hasa iliyopo kwa binadamu na tembo.
Anataja kuwapo maarifa ya jadi na rasilimali za asili, zimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wengi vijijini. Hiyo inatajwa kuendana na changamoto zilizopo zinaboreshwa, pia kusambazwa kwa wakulima wengi, zikiunganishwa na juhudi za serikali na wadau wa uhifadhi, inatajwa kuongeza ufanisi stahiki.
* Mwandishi ni Mtaalamu Hifadhi, pia Mshauri Elekezi wa Miradi ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Uhifadhi. Baruapepe: francisndemela@gmail.com; simu: +255 787441423.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED