Nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job, amesema licha ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu na Kombe la FA, msimu huu ulikuwa mgumu zaidi kwao.
Akizungumza na Nipashe jana, Job, alisema msimu huu ulikuwa na changamoto mbal- imbali na haikuwa kazi rahisi kutetea makombe yao yote.
“Unaweza kuona ilitubidi tusubiri mpaka mchezo wa mwisho kujua kama tutafanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, ki ukweli ulikuwa msimu wenye ushindani na changamogto kubwa sana,” alisema Job.
Aidha, alikiri eneo pekee ambalo hawakuwa sawa na kukosa bahati ni kwenye mashindano ya kimataifa baada ya kuondolewa hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tunaenda kujipanga, naamini msimu ujao tutarejea tukiwa na nguvu na uchu zaidi wa kufanya vizuri kimataifa, lazima tuseme ukweli, msimu huu kimataifa hatukufanya vizuri,” alisema Job.
Alisema, anaushukuru uongozi pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na ushirikiano waliompa tangu alipojiunga na timu hiyo.
“Mashabiki wetu walituonyesha upendo mkubwa katika kipindi chote, walitupa nguvu ya kuendeleza ushindani kwenye michezo yote,” alisema beki huyo anayeichezea pia timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa kwa kukusanya pointi 82 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 78.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED