Mama adaiwa kumuua mtoto wake, ajeruhi wengine wawili

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:53 PM Jul 02 2025
Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro
Picha: Mtandao
Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Zuhura Juma, maarufu Matengo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa miezi saba, Shufaa Abdallah na kujeruhi wengine wawili.

Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, aliyasema hayo juzi na kuwataja majeruhi ni Agnes Mathias na Suleiman Abdala.

Alisema tukio hilo lilitokea Jumatano (Juni 30, 2025), saa sita mchana maeneo ya  Nyumbanyeupe Majimatitu Mbagala, wilayani Temeke.

“Mtuhumiwa anadaiwa alitumia kitu chenye ncha kali kutenda kosa hili. Mauaji ya mama huyu anayetuhumiwa kumuua mtoto wake yamelifanya Jeshi la Polisi kushirikiana na taasisi zingine za kisayansi kuchunguza kisa hili,” alisema.

Kamanda Muliro alisema uchunguzi utakapokamilika taratibu zingine za kisheria zitaendelea.

Mauaji hayo ni mwendelezo wa matukio kadhaa ambayo yamewahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuhusu watu kuendelea kujichukulia hatua na kusababisha vifo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Sheria ya Mtoto Mwaka 2009, ni waraka unaoshughulikia masuala mengi kitaifa yanayohusu haki na ulinzi wa mtoto. Pia inachukua mikataba na makubaliano yanayohusu haki za mtoto kwa ujumla. 

Inalenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za watoto nchini hapa, imeainisha haki ya mtoto kulelewa na wazazi, haki ya kupewa jina kuwa na utaifa, haki ya kupata mahitaji ya msingi kama chakula, malazi, mavazi, matibabu, chanjo, elimu, na haki ya kucheza na kuburudika. 

Licha ya kuwapo kwa sheria hii, matukio ambayo yanaendelea kuripotiwa ni pamoja na lile lililoripitiwa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Ambapo mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Lugubu, Kata ya Lugubu wilayani Igunga, mkoani Tabora, alipoteza maisha pamoja na watoto wake wanne baada ya kunywa sumu aina ya ruruka 80WDG itumikayo kuulia viwaji jeshi.

Katika tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao, alisema mama huyo alinunua pakiti moja ya dawa hiyo ambayo ni sumu ya kuulia wadudu na kuikoroga katika kikombe cha chai kisha akawanywesha watoto wake wote na yeye mwenyewe akanywa, na kuwasababishia umauti.

Mwezi Desemba mwaka jana, jijini Dodoma, kuliripotiwa tukio la mtoto wa mfanyabiashara, Graison Kanyenye (6) ambaye alidaiwa kuuwawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa matembezini. Mwili wake ulikutwa na majeraha shingoni.