Mataifa tajiri duniani yameahidi kusaidiana kutafuta mwarobaini wa kuzisaidia nchi masikini kutua mzigo wa madeni, huku Uhispania ikiahidi kupeleka dola bilioni 1.9 (zaidi ya Sh. Trilion 4.9) katika Shirika la Fedha la Kimataifa, (IMF) kusaidia nchi zinazoendelea.
Ahadi hiyo ilitolewa jana baada ya kuhitimishwa kwa kongamano la kimataifa la ufadhili kwa ajili ya maendeleo lililokuwa likifanyika nchini Uhispania, ambako zaidi ya mataifa 100 yalihudhuria.
Ilielezwa kuwa katika hatua ya mataifa hayo kutafuta futa suluhu ya kile walichokitaja kama ‘bomu linalosubiri kulipuka’ kwa kuzingatia mzigo wa deni unaozidi kuyaelemea mataifa yanayoendelea, ingawa yalijikuta kwenye mgawanyiko kuhusiana na namna watakavyolitekeleza hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres aliuambia mkutano huo kwamba mzigo wa madeni unaulemaza ulimwengu unaoendelea, na kusisitiza nguvu ya pamoja katika kuyasaidia mataifa hayo yenye kipato cha chini kujiondoa kwenye changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa UN, deni la nje la nchi masikini zaidi limeongezeka zaidi ya mara tatu katika kipindi cha miaka 15.
Ilielezwa kuwa mataifa yanayoendelea kwa sasa yanalazimika kuwalipa wakopeshaji dola trilioni 1.4 kila mwaka kulingana na masharti ya mkopo, kiwango kilichoongezeka katika miaka 20. Na kwamba mataifa masikini pia yanakabiliwa na mzigo wa riba ambao ni mara mbili zaidi ya mataifa tajiri.
Kwa mujibu wa ripoti iliyoagizwa na hayati Papa Francis na kuratibiwa na mwanauchumi na mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Nobel Joseph Stiglitz, zaidi ya watu bilioni tatu wanaishi katika nchi ambazo hulipa fedha nyingi kwenye riba kuliko zinazoingizwa kwenye sekta ya afya.
Waziri wa Uchumi wa Uhispania Carlos Cuerpo aliiambia Reuters pembezoni mwa kongamano hilo kwamba taifa hilo litaendelea kuwa mfano katika mchakato wa kupata suluhu kwa kutoa sehemu ya fedha kwa maslahi ya mataifa yanayoendelea.
Aidha, ilielezwa kuwa hatua hiyo ya Uhispania inalingana na juhudi pana za wafadhili za kusaidia nchi zenye mahitaji, na hasa baada ya Marekani aliyekuwa mfadhili mkuu kukataa kuunga mkono mpango kazi uliofikiwa kwenye mkutano wa kilele wa mwaka jana.
Rais wa Kenya William Ruto na Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, miongoni mwa viongozi wa Afrika walioshiriki katika kongamano hilo walitoa wito wa mageuzi kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa ili kutatua changamoto ya mzunguko huo mbaya wa kifedha.
Waraka uliopitishwa na washiriki unataka kupitishwa kwa vifungu vya mikopo vitakavyoruhusu nchi zinazokopa kusimamisha kwa muda kurejesha mikopo kutokana na athari kama maafa ya asili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED