Diogo Jota afariki kwa ajali ya gari

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:35 PM Jul 03 2025
Diogo Jota (28)
Picha: Mtandao
Diogo Jota (28)

Dunia ya soka imepigwa na butwaa kufuatia taarifa za msiba wa ghafla wa mshambuliaji wa Kimataifa wa Ureno, Diogo Jota (28), aliyefariki dunia katika ajali mbaya ya gari.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kikosi cha kijeshi cha Hispania, Guardia Civil, ajali hiyo ilitokea katika eneo la Rionegro del Puente, ambapo Kituo cha Zimamoto cha eneo hilo kilithibitisha kuwa ajali hiyo ilisababisha vifo vya vijana wawili wenye umri wa miaka 28 na 26.

"Gari hilo lilishika moto mara baada ya ajali na moto huo ukaenea hadi kwenye mimea ya jirani. Vijana hao walikuwa wamekwama ndani ya gari na walifariki papo hapo," ilieleza taarifa ya Zimamoto.

Safari ya Soka ya Jota

Jota alianza kucheza soka katika nchi yake ya Ureno kupitia akademi ya Pacos de Ferreira kabla ya kujiunga na klabu ya Atletico Madrid ya Hispania mnamo mwaka 2016. Hata hivyo, hakuwahi kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo ya LaLiga, na badala yake alitolewa kwa mkopo kwenda FC Porto — klabu ya mji alikozaliwa — kisha akaelekea Wolverhampton Wanderers (Wolves) mwaka 2018.

Alitamba kwa misimu miwili akiwa chini ya kocha mwenzake wa Kireno, Nuno Espirito Santo, kabla ya kusajiliwa rasmi na Liverpool mnamo Septemba 2020.

Akiwa Liverpool, Jota aliibuka kuwa mmoja wa washambuliaji mahiri, akichangia mafanikio kadhaa ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (Premier League), Kombe la FA na Kombe la Carabao. Pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2021/2022, ambapo Liverpool ilipoteza dhidi ya Real Madrid kwa bao 1-0, Jota akicheza kama mchezaji wa akiba.

Safari ya Kimataifa

Jota aliitumikia timu ya taifa ya Ureno kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2019. Alishiriki michuano ya Euro 2020 na Euro 2024. Hata hivyo, alikosa Kombe la Dunia la mwaka 2022 kutokana na jeraha.

Kwa jumla, alifanikiwa kutwaa taji la UEFA Nations League mara mbili akiwa na kikosi cha Ureno, ikiwemo toleo la hivi karibuni lililomalizika Mei mwaka huu.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa si tu kwa familia na mashabiki wake, bali pia kwa dunia nzima ya soka ambayo bado ilihitaji mengi kutoka kwake. Mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu, mwenye nidhamu na moyo wa ushindani — Diogo Jota atakumbukwa daima.