MUHITIMU wa kidato cha sita aliyeshindwa kujiunga na chuo cha ualimu kwa kukosa ada, Bernard Mwakajila ametengeneza ‘A’ 1OO za somo la hisabati katika shule ya Sekondari Kimara iliyopo Wilayni Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Mhitimu huyo, anasema aliingia katika shule hiyo kwa lengo la kusaidia wanafunzi wengi kufaulu somo hilo, ikiwa ni sehemu ya ndoto zake tangu akiwa shuleni.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii katika mahojiano maalum huko shuleni kwao juzi, Mwakajila ambye pia ni maarufu kwa jina la “Mgalatia wa Hesabu” anasema yeye ni miongoni mwa waliologwa na somo hilo.
Katika simulizi yake anasema kati ya wanafunzi wake 457 waliofanya mtihani wa taifa kidato cha pili mwaka jana kati yao 100 walifaulu somo la hisabati.
Anaposimulia namna alivyofanikisha kufaulisha wanafunzi wengi katika somo hilo, mwalimu huyo anaamini jambo la kwanza ni kumtanguliza Mungu mbele pamoja na ushirikiano mzuri kati yake, wanafunzi na uongozi wa shule.
“Ninapofana kazi katika mazingira mazuri ninakuwa sawa kabisa kufundisha hisabati, kwahiyo kutokana na mazingira mazuri yaliyopo katika shule hii, wote tukajikuta tunaimba wimbo mmoja lazima tufanye vizuri kwenye hesabu” anasema Mwakajila huku anasisitiza hilo pia limetokana na juhudi za pamoja
Mwakajila ambaye alitunukiwa tuzo ya kuwa mwalimu bora wa hisabati Wilaya ya Ubungo na hata kufanikiwa kutoa mwanafunzi bora katika somo hilo, anasema kutofanya vizuri kwa shule nyingine kunatokana na kukumbatia ile dhana ya kwamba somo hilo ni gumu ‘ugonjwa wa taifa’ kitu ambacho siyo kweli.
“Ile dhana ya kusema hesabu ni ugonjwa wa taifa ile hali inapokaa kichwani kwa mwanafunzi na mwalimu akashindwa kuiondoa hilo ni tatizo…, ili kufanikisha wanafunzi wafanye vizuri katika somo hilo lazima mwalimu awe mwanafunzi kwa kuwa na muda wa ziada wa kutafuta mbinu za kumfanya alijue na alipende somo hilo.
“Lazima uwe na muda wa ziada wa kuwasoma wanafunzi darasani na kugundua kila mwanafunzi mmoja mmoja anashida gani kwenye eneo gani kwa haraka na kumsaidia lakini kama hufanyi hivyo itakuwa ngumu.
“Kwa mfano katika darasa langu, niliwasoma jinsi wanafunzi wangu walivyokuwa na uwezo wao nikawaambia walimu wenzangu kwamba kwa jinsi ninavyoliona hili darasa ninaweza kupata ‘A’ 100 na niliamini hilo na imewezekana.
“Lakini pia mwaka 2021 nilitengeneza ‘A’ 49 kwa wanafunzi wa kidato cha pili kwahiyo nilicho kifanya mwaka jana ni mwendelezo wa kile nilicho kifanya mwaka huo” anasema mwalimu huyo
Mwakajila anasema kutopata daraja ‘A’ kwa wanafunzi wengine katika darasa lake kumetokana na namna Mungu alivyowaumba binadamu na utofauti wake kwamba kuna mwanafunzi ambaye hata ungemfundisha vipi hawawezi kuelewa na kwamba halaumu sana bali anaendelea kuona namna ya kuongeza juhudi wote wafanikiwe.
Anaitaja moja ya mbinu aliyotumia kufanikisha wanafunzi hao kulipenda somo la hisabati na hata kufanya vizuri kuwa ni pamoja kuwapa zawadi ndogondogo wale wanaofanya vizuri kwa grade yake.
Anatolea mfano kwamba mwanafunzi aliyekuwa anatoka kwenye daraja F kuja D alikuwa anampa motisha ya Sh 1,000 vilevile kwa aliyekuwa natoka D kwenda C, B na A.
Anasema pia anapoletewa hesabu ambayo imemshinda mwanafunzi huwa anaenda kuifanya mbele ya wanafunzi wenzake darasani, kwa njia nyepesi na mwalimu pia anatakiwa kuwa na mbinu nyingi za kufanya maswali.
Mbali na somo la hisabati mwalimu huyo anasema ni mtaalamu pia katika somo la phizikia japo, katika shule hiyo amepewa jukumu la kufundisha hisabati pekee huku akibainisha kuwa siku uongozi wa shule ukimpa jukumu la kufundisha pia somo hilo yupo tayari kwa sabbau yeye amesoma mchepuo wa PCM.
OMBI LAKE
Mwalimu huyo anasema: “Ninafanya haya yote lakini sijapita chuo cha ualimu mimi nimetokea moja kwa moja kidato cha sita nilifaulu kwenda chuo lakini nilikosa ada… niaomba serikali, wadau binafsi wanisadie niweze kusoma chuo ili niwe mwalimu mwenye vyeti niendelee kutumika kusaidia wanafunzi wengi kupenda na kufaulu somo la hesabu" anawasilisha rasmi ombi lake Mwakajila
Kutokana na jitiha zake mwalimu huyo anasema alitunukiwa tuzo shuleni kwake iliyotolewa na walimu wenzake, pia Mkurugenzi Manispaa ya Ubungo alimtambua kama mwalimu bora wa hesabu katika wilaya hiyo.
“Siku ya elimu iliyofanyika Ubungo nilipewa tuzo ya kunitambua kama mwalimu Bora wa hesabu na mwanafunzi bora wa katika hilo alitoka katika darasa langu kwahiyo Mkurugenzi wa Ubungo anafahamu na anajua jitihada zangu” anasema mwalimu huyo
NINI MALENGO YAKE?
Mwalimu huyo anasema anatamani kuja kuwa na shule ambayo msingi wake mkubwa utakuwa somo la hisabati pamoja na kuondoa dhana ya kwamba somo hilo ni gumu.
Anasisitiza atakapopata mafanikio hayo, atashirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na wadau kuondoa hiyo dhana ya hesabu kuonekana kama ni somo gumu ili wapatikane wagalatia wengi wa somo hilo.
“Hesabu ni sanaa ya namba ninatamani serikali itengeneze klabu za hisabati ili kuzalisha walimu wazuri nguvu iongozwe zaidi kuzalisha wagalatia wengine kwa mfano hawa wanafunzi 100 nilio watengeneza waendelezwe ili tupate walimu wengi zaidi wa hesabu” anasisitiza mwalimu huyo
WANAFUNZI
Munira Maliki miongoni mwa waliopata ‘A’ anasema alipokuwa anaanza kidato cha kwanza alikuwa anaamini somo hilo ni gumu lakini alipokutana na mwalimu huyo alimuaminisha kwamba somo hilo ni jepesi kwa kumpa maneno yenye hamasa wakati wote.
Anasema atahakikisha anapata 'A' nyingine ya hesabu akiwa kidato cha nne kama ataendelea kufundishwa na mwalimu huyo kwakuwa wanamuelewa vizuri.
Munira mwenye ndoto ya kuja kuwa daktari anasema hilo litatimia kwa kufanya vizuri katika hesabu na masomo mengine ya sayansi.
Mwanafunzi mwingine aliyefanya vizuri katika somo hilo, Jackson Warioba alisema kufanikiwa kwake kumetokana na ushirikiano katika yake na walimu.
Anasema wanoona hesabu ngumu sio kweli akiwa na ushauri kwamba ili mwanafunzi afanikiwe katika somo hilo lazima asome kwa bidii na kufanya mazoezi kila wakati.
“Haikuwa ngumu sana kumwelewa mwalimu mpaka kufaulu hisabati mwalimu alikuwa anatuelekeza vizuri mpaka unaelewa kitu kwa makini kabisa” anasema Jackson ambaye pia alitunukiwa tuzo kama mwanafunzi aliyefanya vizuri katika somo hilo Wilayani Ubungo
MKUU WA SHULE
Mkuu wa Shule hiyo, Leticia Malosha anasifu uwezo wa mwalimu huyo umesaidia kubadili mtazamo wa wanafunzi na kuamini somo hilo ni jepesi hali ambayo imepelekea wakafanya vizuri katika mtihani mwaka jana.
“Mwanzoni hata Mimi nilikuwa ninaamini hesabu ni ngumu lakini alipokuja hapa akatubadili mtazamo na ameweza kutusaidia kuapata ‘A’ 100 katika somo hilo japo anajitolea.
Hata hivyo mkuu huyo wa shule anasema, anatamani mwalimu huyo apate ufadhiri kutoka serikalini au watu binafsi aende chuo ili awe mwalimu kitaaluma kwa kuwa meshindwa kufikia ndoto hiyo kutokana na uwezo wa kifedha kwa sababu anakipaji kikubwa sana cha kufundisha hesabu.
“Fikiria anauwezo mkubwa wa kufundisha hesabu na hajapita chuo cha ualimu, kwahiyo ipo haja apatiwe msaada ili alitumikie taifa letu” anasema mwalimu huyo
Mwisho
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED