Mgombea mwenza wa kiti cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuzindua rasmi kampeni za chama hicho ngazi ya mkoa wa Mwanza kesho, Agosti 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa, amesema mkoa huo umepata heshima ya kuwa wa pili kuandaa uzinduzi wa kampeni hizo ambazo zitafanyika katika viwanja vya Furahisha, wilayani Ilemela.
“Wananchi wa Mwanza watarajie kampeni za kistaarabu, zitakazonadi sera na kueleza namna serikali ya CCM itakavyotekeleza mipango yake katika kipindi kijacho cha miaka mitano,” amesema Mtuwa.
Aidha, aliwasihi wanachama wa CCM walioshiriki katika mchakato wa kura za maoni lakini hawakufanikiwa, kuungana na chama na kuepuka kuvunja makundi.
“Kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chetu, makundi yalishaisha tangu Agosti 22, 2025 baada ya uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani. Sasa tuna kundi moja tu la CCM, tuungane kuhakikisha ushindi wa chama chetu,” ameongeza Mtuwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED