DC Mtatiro ahamasisha wananchi kuchangia maendeleo

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 01:21 PM Aug 28 2025
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa kuanzisha miradi ya ujenzi wa maboma, ambayo serikali itamalizia na kuanza kutoa huduma muhimu.

Kauli hiyo Mtatiro ameitoa wakati akisikiliza kero za wananchi katika Kata za Lyamidati, Lyabukande na Mwakitolyo, akiwa ameambatana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali.

“Mimi hufurahia sana kuona wananchi wakichangia shughuli za maendeleo, ikiwamo kuanzisha ujenzi wa maboma. Nawapongeza wananchi wa Kijiji cha Kizungu, Kata ya Lyamidati, kwa hatua ya kujenga shule shikizi ya Matogoro. Nawahakikishia serikali itamalizia ujenzi huo, ninyi mtoe tu kwenye renta,” amesema Mtatiro.

Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa kero zote walizowasilisha zitatatuliwa, huku akiwataka wataalamu na viongozi wa taasisi za serikali kutoa mrejesho wa maandishi kuhusu utekelezaji wa changamoto hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mwita Waryuba, amesema serikali itatoa Sh milioni 5 kuendeleza ujenzi wa shule hiyo na ikifika hatua ya renta itamaliziwa ili huduma zianze kutolewa.

Akizungumzia kero ya upungufu wa watumishi wa afya, Waryuba amesema hilo ni tatizo la kitaifa, na kwamba ajira zitakapokuwa zikitolewa, watakuwa wakiwagawa kwa uwiano sawa.

“Kero zote ambazo zimewasilishwa na wananchi, zingine tayari zipo kwenye mipango ya utekelezaji na zimetengewa bajeti, na zote zitatatuliwa kama alivyoelekeza Mkuu wa Wilaya,” ameongeza.

Naye wananchi, kwa nyakati tofauti, waliwasilisha kero zao ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa maji safi na salama, huduma za umeme, upungufu wa watumishi pamoja na kutopatikana kwa mtandao wa simu.