Tanzania yaingia makubaliano kimataifa kudhibiti kemikali hatari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:53 PM Aug 28 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo katika Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya (IDEC39).

TANZANIA imeingia makubaliano na nchi zinazozalisha kwa wingi kemikali bashirifu ili kudhibiti kemikali hatari zinazotumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya.

Hayo yalielezwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya (IDEC39). 

Mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA) ulifanyika kuanzia Agosti 26 hadi 28, mwaka huu jijini Nashville nchini Marekani.

“Pia, Tanzania imepata nafasi ya kujadiliana na nchi zinazozalisha mmea wa Kratom unaotengeneza dawa mpya ya kulevya aina ya ‘Mitragyna Speciosa’ na kuridhiana njia bora ya kushirikiana kudhibiti dawa hiyo ambayo hata katika nchi hizo imeorodheshwa kama dawa hatari ya kulevya inayodhibitiwa,” alisema.

Awali siku chache zilizopita mamlaka hiyo nchini ilifanikiwa kukamata zaidi ya tani 30 ya aina mpya ya dawa ya kulevya ‘Mitragyna Speciosa’ ambazo ziliingizwa nchini, huku wahusika ambao wako kizuizini wakidai kuwa ni mbolea.

1
Kupitia ushiriki huo, Kamishna Jenerali Lyimo alisema, Tanzania imenufaika kwa kiwango kikubwa, jambo linaloonesha matunda ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia.

Alisema, mkutano huu muhimu umewakutanisha viongozi wakuu wa mamlaka za udhibiti wa dawa za kulevya kutoka mataifa mbalimbali duniani, lengo likiwa ni kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kupambana na uhalifu wa kimataifa unaohusisha dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema, ujumbe wa Tanzania umepata uzoefu kutoka kwa nchi zinazotengeneza vifaa vya kisasa vya kubaini dawa za kulevya, jambo litakalosaidia kuimarisha udhibiti na usalama katika mipaka.

“Mkutano huu umeonyesha umuhimu wa kuongeza nguvu katika kudhibiti biashara ya dawa za kulevya inayoendelea kuhamia katika majukwaa ya kidijitali, kwa kushirikisha sekta binafsi.

“Pamoja na hayo, nchi washiriki wamejifunza na kukumbushwa umuhimu wa kuwekeza katika upelelezi wa kisayansi kupitia ‘forensic intelligence’.

“Dunia kwa sasa inashuhudia mbinu mpya za kutengeneza dawa za kulevya, ambazo zinapita nje ya mifumo ya kawaida, hali inayotishia ufanisi wa mbinu za zamani za udhibiti.

“Hii ina maana kwamba, uwekezaji katika teknolojia na sayansi ni muhimu zaidi ili kuendelea kufanikisha vita hii. Kupitia mkutano huu, Tanzania imepata ushirikiano mpya na nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa,” alisema Kamishna Lyimo.

MAFANIKIO

Alisema mojawapo ya mafanikio waliyoyapata ni makubaliano na shirika kubwa la kimataifa la INL, ambalo limeahidi kushirikiana na DCEA kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa kutumia vifaa vya kisasa hususani kuimarisha Maabara ya Vipimo vya Kibaiyolojia katika masuala ya jinai.

Pia, kikao muhimu kimefanyika kati ya Kamishna Jenerali Aretas Lyimo na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Nigeria (NDLEA), Brigedia Jenerali Maro, ambako wamekubaliana kuharakisha makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Nigeria katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Taifa katika kulinda usalama wa wananchi na kuimarisha uchumi kupitia mapambano thabiti dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kujali utu na kulinda afya za watanzania.

Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha vijana wa Tanzania wanalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.