Wagombea 17 ubunge Kigamboni wateuliwa, wenye pingamizi waitwa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 10:36 AM Aug 28 2025

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigamboni, Selemani Kateti.
Picha: Mpigapicha Wetu
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigamboni, Selemani Kateti.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigamboni, Selemani Kateti, amesema wagombea wote 17 wa nafasi ya Ubunge waliokuwa wamechukua fomu za uteuzi, wamerejesha fomu hizo na tayari zimebandikwa kwa mujibu wa taratibu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kufunga mchakato wa kupokea na kubandika fomu hizo, Kateti alisema vyama vyote vilivyoshiriki vilifuata utaratibu, na wagombea wote wameteuliwa rasmi kuwania nafasi hiyo.

“Mchakato ulianza saa 1:30 asubuhi hadi saa 10 jioni, (jana) na fomu zimebandikwa kuanzia muda huo hadi kesho saa 10 jioni (leo). Kama kutakuwa na pingamizi kwa wagombea, tutapokea kwa mujibu wa taratibu,” alisema Kateti.

Alibainisha kuwa zoezi lote limeenda vizuri bila changamoto au malalamiko, ambapo wagombea wote walirejesha fomu zao mapema kuanzia asubuhi.

Kwa mujibu wa Kateti, mamlaka zenye haki ya kuwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea ni pamoja na wagombea wa ubunge wa jimbo husika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Kwa utaratibu, atakayeleta pingamizi atajaza fomu namba 9B akieleza sababu, na kuiwasilisha kwa msimamizi wa uchunguzi,” alisema Kateti.

Amefafanua kuwa kuna jumla ya sababu 16 zinazoweza kusababisha pingamizi kwa mgombea, ikiwemo endapo mgombea si raia wa Tanzania, amewahi kutiwa hatiani kwa kosa la kukwepa kodi, au hajalipa dhamana ya shilingi 50,000.

Aidha, Kateti aliongeza kuwa mgombea atakayekumbwa na pingamizi ana haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.