"Hakuna taratibu zozote zilizokiukwa kumpata mgombea urais CCM"

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 05:31 PM Aug 28 2025
Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.
Picha: Nipashe Digital
Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.

Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amesema hakuna taratibu zozote zilizokiukwa katika kumpata Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa chama hicho, akisisitiza kuwa CCM kimeendelea kuheshimu utaratibu wake wa ndani tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Parkers, Dar es Salaam, Dk. Kikwete amesema malalamiko na maneno ya kejeli kutoka baadhi ya watu hayana msingi.

“Na mimi nililaumiwa nilivyosema kwenye Mkutano Mkuu. Waliosema hayo ama hawajui utaratibu wa chama, au wamesahau, au wanajifanya hawajui. Tangu tumeanza mfumo wa vyama vingi, Rais aliyepo madarakani akimaliza kipindi cha kwanza na akitaka cha pili huwa anapewa nafasi. Ndivyo ilivyokuwa kwa (Benjamin) Mkapa, kwangu na kwa Rais (John) Magufuli. Kwa nini leo alipotaka Samia kuwe na kelele? Sababu yake nini?” amehoji Kikwete.

Ameongeza kuwa watu wanaopinga au kutia shaka utaratibu huo ni wale wenye “kimbelembele” ambao pia walikuwepo wakati wa marais waliomtangulia, lakini sasa wanataka kuwapa hofu wanachama na Watanzania bila sababu.

Dk. Kikwete amesema mwangwi wa kauli ya “Samia mitano tena” umetokana na wananchi kuridhishwa na kazi kubwa aliyofanya katika miaka yake mitano ya uongozi, akisisitiza kuwa alipoapishwa Machi 19, 2021, alikabidhiwa nchi katika mazingira magumu baada ya kifo cha Rais John Magufuli.

“Nadhani tulikumbuka maneno yale—hivi huyu mama ataweza kweli kuongoza nchi? Lakini wewe ulitupa matumaini na kuondoa hofu. Rais ni taasisi, haina jinsia. Umetuonesha kuwa unayajua majukumu yako na umeweza kuyatekeleza kwa weledi,” amesema Kikwete.

Ameongeza kuwa Samia ameiongoza nchi vizuri, akidumisha amani, utulivu, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza miradi ya maendeleo.

“Marais tuliopita tulikuwa na muda wa kutengeneza timu zetu, sera na mikakati kabla ya kuingia madarakani. Lakini mama Samia alijikuta ghafla ni Rais bila maandalizi, akiwa ziarani Tanga akaletewa taarifa ya msiba wa Rais. Hali ile ilikuwa ngumu sana. Lakini aliingia kama komando aliyerushwa katikati ya maadui huku akipiga risasi, na amedhibiti mazingira ipasavyo,” amesema Kikwete.