CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimewataka watiania wa chama hicho waliokatwa katika mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwa ajili ya kupeperusha bendera kwenye Uchaguzi Mkuu wasifanye nongwa kuna nafasi nyingi watapewa.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Khamis Mbeto, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi kuu za CCM Kisiwandui, visiwani humo.
Mbeto alisema nafasi zipo nyingi, ikiwa mtu hajateuliwa katika nafasi hizo atapewa nyingine ambayo inamtosha na inamfaa kwa wakati huu.
“Wale ambao wamepata nafasi za kuteuliwa kupeperusha bendera yetu katika uchaguzi mkuu tunawapongeza na wale ambao hawajateuliwa pia tunawapongeza, wajue kuwa chama kina nafasi nyingi kinaweza kuwatumia katika maeneo mbalimbali,” alisema Mbeto.
Alisema katika mchakato huo wa kuwapata wagombea, Kamati Kuu ya CCM imefanya haki, imechunguza na kuangalia katika maeneo mbalimbali kwasababu chama kinataka viongozi wanaokubalika katika jamii na wasiotiliwa shaka na mambo yoyote yale ikiwamo rushwa na maadili.
Aidha, alisema chama kinahitaji viongozi watakaokisaidia ili kushinda katika uchaguzi na kuwakilisha katika vyombo vya dola.
Alisema mchakato wa CCM upo kihalali na unaotenda haki na kuna wanaCCM waligombea miaka mitano iliyopita na walikatwa, lakini mara hii wameteuliwa ina maana ya kuwa wapo safi na wamerekebisha upungufu wao.
Mbeto alisema CCM ina utaratibu na mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni katika chama sio suluhisho ya kuwa ni kigezo kuwa aliyepata kura nyingi ndio mshindi, huo sio uteuzi wa mwisho.
“CCM inapotaka kuteua mtu lazima ifanye uchunguzi na kujiridhisha na mgombea na fungu la nne la kanuni la uteuzi la viongozi wa dola ndani ya CCM. Mgombea tunaempeleka kwanza uanachama wake usitiliwe shaka, mgombea anayekubalika na jamii,” alisema.
Alisema zipo sababu nyingi za kukatwa kwa wagombea ikiwamo za kimaadili, lazima kupata viongozi ambao wanamaadili mazuri kwa sababu baadhi ya watiania wameondolewa kwa ulevi wa kupindukia na kutokuwa na staha katika mambo yao ya faragha.
Alipiga marufuku kwa mgombea yeyote ndani ya chama aliyepitishwa katika mchakato huo kufanya sherehe na atakayebainika atapelekwa katika kamati ya maadili ya chama na kamati haitosita kumwengua.
Akizungumzia kuhusu mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema anatarajiwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo Agosti 30, mwaka huu katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zilizopo Maisara.
Alisema uchukuaji utafanyika majira ya saa 4:00 asubuhi na atakwenda na viongozi wachache akiwamo mwanasheria wa CCM ili kufuata taratibu za ZEC kuwa hakitaki shangwe.
Alisema baada kuchukua fomu nje ya Ofisi za ZEC atapokewa kwa shangwe na wafuasi wa CCM na akitoka hapo, CCM imeandaa gari maalum la wazi atakaloingia mgombea na kupita katika barabara ya Maisara, Magereza, Miembeni na Michenzani hadi ofisi kuu za CCM, Kisiwandui.
Atakapofika Kisiwandui atakwenda kuomba dua katika kaburi la Rais wa Kwanza, Hayati Abeid Amani Karume na kisha atazungumza na wazee wa CCM ofisi za Kisiwandui.
Aidha, Dk. Mwinyi ataekelea katika viwanja vya Maozedding na kulakiwa na wafuasi wa CCM.
ARUSHA
Mgombea Ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amechukua fomu ya kugombea kiti hicho katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku akitaja mambo matatu yanayofanya kuandika jina lake kwa wino wa dhahabu, ikiwamo kupakwa mafuta na kupata kibali cha kuteuliwa kuwa mgombea.
Makonda, aliyasema hayo jana jijini Arusha, muda mfupi baada kukabidhiwa fomu ya kugombea nafasi hiyo.
"Ukizaliwa na kusoma Kanda ya Kaskazini, oa au olewa ukanda huu ili ufanikiwe, lakini usisahau kumcha Mungu. Ni suala laupendo, amani na utulivu na tutafanya kampeni za kistaarabu ," alisema Makonda.
Aidha, mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, kupitia CCM, Enock Koola, amesema kuwa wakati wa makundi umefika mwisho na sasa ni wakati wa kupambania ushindi.
Baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),
Akizungumza kuhusu mwenendo wa uchukuaji fomu za uteuzi, Msimamizi wa uchaguzi Majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo Lucas Msele, alisema kuanzia Agosti 14 hadi jana Agosti 26 majira ya saa nane mchana jumla ya vyama 19 vimechukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge katika majimbo hayo, vyama tisa ni Jimbo la Moshi Vijijini na 10 Jimbo la Vunjo.
"Kwa Jimbo la Moshi Vijijini vyama vilivyochukua fomu mpaka sasa ni pamoja na CUF, CCK, ADATADEA, TLP, CHAMA CHA DEMOKRASIA MAKINI, ACT WAZALENDO, CHAUMMA na CCM huku Jimbo la Vunjo ikiwa ni DP, ACT WAZALENDO, ADATADEA, CHAMA CHA DEMOKRASIA MAKINI, CCK, AFP, TLP, CHAUMMA, NRA na CCM" alisema Msele.
TARIME
Huko Tarime, msafara wa kumpokea Esther Matiko kwenda kuchukua fomu umepata ajali na kusababisha kifo huku yeye akipata majeraha kwenye mkono na kichwani.
Aidha, mtoto wa mjomba wake, Kisanta Ghati na mdogo wake, Mrimi Matiko, pia walijeruhiwa wakati wakimsindikiza kwenda kuchukua fomu ya ubunge Jimbo la Tarime Mjini.
KILINDI
Mgombea ubunge wa Jimbo la Lupembe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edwin Swalle, amechukua fomu ya kugombea kwa mara nyingine ili kutetea nafasi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Swalle alivitaka vyama vya upinzani kujiandaa na changamoto kubwa, akisisitiza kuwa “watapata tabu sana.”
Alisema kuwa katika kampeni zake na utekelezaji wa ilani, ataanzia pale alipoishia, akilenga kuendeleza juhudi za kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Lupembe.
Wagombea wengine waliochukua fomu ni Daniel Chongolo wa Jimbo la Makambako ambaye alisindikizwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Deo Sanga (Jah People) na huku Deo Mwanyika akichukua katika Jimbo la Njombe Mjini.
Wakati huo huo, Chama cha ACT – Wazalendo, Joma Mwakisitu amechukua fomu ya kugombea jimbo la Makete na kuahidi kushughulikia changamoto za kilimo, wa Chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA, Sigrada Mligo amechukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo la Njombe mjini.
*Imeandaliwa na Rahma Suleiman (ZANZIBAR), Godfrey Mushi (ARUSHA), Eliza John (KILINDI) na Samson Chacha (TARIME)
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED