SAU yazindua mabango kumnadi mgombea wake

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 06:53 PM Aug 28 2025
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Majalio Kyara, akizungumza na baadhi ya wakazi wa jiji la Dodoma mara baada ya kuzindua uwekaji mabango kwa ajili ya kumnadi mgombea huyo kuelekea uchaguzi mkuu 2025.
Picha: Paul Mabeja
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Majalio Kyara, akizungumza na baadhi ya wakazi wa jiji la Dodoma mara baada ya kuzindua uwekaji mabango kwa ajili ya kumnadi mgombea huyo kuelekea uchaguzi mkuu 2025.

Chama Cha Sauti ya Umma (SAU) kimezindua rasmi zoezi la uwekaji mabango kwa ajili ya kumnadi mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo, Agosti 28, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo, mgombea wa urais kupitia chama hicho, Majalio Kyara, alisema zoezi hilo litaendelea nchi nzima.

“Hapa Dodoma ni sehemu ya uzinduzi wa kitaifa, na kwa siku ya leo tumeweka mabango 107. Tutakwenda pia katika mikoa yote nchini kuweka mabango haya ambayo sasa ni rasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” amesema Kyara.

Aidha, ametangaza kuwa chama hicho kitazindua rasmi kampeni zake za kitaifa wilayani Temeke, Dar es Salaam, eneo la Ngongolamoto mnamo Septemba 9, 2025.

“Kabla ya uzinduzi wa kampeni, tutazindua ilani ya chama chetu kwa njia tofauti na vyama vingine ili Watanzania wapate kuelewa vyema sera na mipango yetu,” ameongeza Kyara.

Kwa mujibu wa Kyara, kampeni za SAU zitaendeshwa kwa mbinu mbalimbali ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii, kampeni za nyumba kwa nyumba na mikutano midogo midogo ya hadhara katika maeneo ya mikusanyiko.