MAZIWA ya mama yana virutubisho vyote muhimu, mtoto anahitaji katika miezi sita ya kwanza ya maisha, ikiwamo protini, mafuta, pia ni chakula kamili kwa mtoto mchanga.
Zipo faida 10 zinazotajwa na wataalam wa afya ambazo mtoto anapata kutokana na kunyonya maziwa ya mama, ikiwamo kupanua wigo muhimu kwa maendeleo ya afya mama na mtoto.
Vilevile, maziwa ya mama yanatajwa kuwa na virutubisho bora kwa mtoto anayekua na kuongeza uwezo wa ubongo, hatua inayotakwa kuweza kupunguza hatari ya saratani na magonjwa mengine.
Takwimu za za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kimataifa viwango vya unyonyeshaji wa watoto vimeendelea kuimarika, idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee imeongezeka, kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022.
Aidha takwimu hizo zinataja idadi ya watoto wanaonyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, imeongezeka nchini kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 70 mwaka 2022 na kwamba hatua hiyo inatia matumaini.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya), Profesa Tumaini Nagu, ambaye kitaaluma ni daktari, anasisitiza hatua zaidi za kuboresha unyonyeshaji wa mama.
Ni hafla ya jijini Dar es Salaam, iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutibu Ukondefu na Uvimbe Unaotokana na Ukondefu MJkali,
Tukio hilo la hivi karibuni ulishirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya lishe, akitaja mafanikio na upungufu kwenye suala la watoto kunyonya maziwa ya mama zao.
"Pamoja na hatua hiyo ambayo Tanzania imepiga, kuna haja ya kuendelea kuimarisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama, ili kusaidia kutokomeza ukondefu na ukondefu mkali kwa watoto," anasema.
Kabla ya kuhamia wizarani, Profesa Nagu, alikuwa mwanataaluma aliiyeongoza Idara ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
KWANINI ANGALIZO?
Profesa Tumaini, anasema pamoja na mafanikio katika kulinda, kuhamasisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama, bado unyonyeshaji haujafikia viwango vinavyoridhisha.
Naibu Katibu Mkuu huyo anasema, asilimia ya watoto wanaoendelea kunyonya maziwa ya mama, hasa wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi miwili imekuwa ikipungua.
"Ni asilimia 35 tu ya watoto wenye umri wa miezi 20 hadi 24 ambao bado wananyonyeshwa, badala yake wanapewa vyakula vingine ambavyo havitoshelezi mahitaji ya lishe ya mtoto," anasema.
Anataja changamoto kubwa zinazowakumba watoto kwa kutonyonyeshwa ipasavyo, ni utapiamlo hasa ukondefu.
Naibu Katibu Mkuu huyo, anadokeza vyanzo vyake vinajumuisha kutozingatia taratibu sahihi za unyonyeshaji na umendelea kuathiri lishe na afya ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano duniani kote.
"Takwimu za mwaka 2022 za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kuwa asilimia 6.8 ya watoto wa kundi hilo, sawa na wwatoto milioni 45, wanakabiliwa na ukondefu, huku asilimia 2.1 wakikabiliwa na ukondefu mkali," anasema.
Anafafanua kwamba Tanzania kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti wa Hali ya Afya na Viashiria vya Malaria Tanzania Demographic and Health Survey- Malaria Indicator Survey ya mwaka 2022), imepiga hatua.
Anasema Tanzania imeweza kufikia viwango vya shirika hilo lililoelekeza kiwango cha ukondefu miongoni mwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika nchi mbalimbali kisizidi asilimia tano,
Inarejea kiwango cha ukondefu kwa watoto hao nchini, kimedhibitiwa na kufikia asilimia tatu tu ambayo imekidhi kiwango cha WHO.
"Kwa kuzingatia idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kiwango hiki ni sawa na watoto 620,000. Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na ukondefu," anaeleza.
Anataja moja ya hatua hizo kuwa ni kuwapo kwa mwongozo wa usimamizi jumuishi wa matibabu ya utapiamlo mkali (Integrated Management of Acute Malnutrition- IMAM 2018), ulioboreshwa.
"Mwongozo huu umeendelea kuhuishwa mara kwa mara ili kuendana na matokeo ya utafiti na ushahidi wa kisayansi uliopatikana kwa nyakati za sasa na uzoefu wa utekelezaji wa huduma za matibabu ya utapiamlo mkali hapa nchini," anasema.
MATUMAINI YA WADAU
Mkurugenzi Mkazi wa shirika Action Against Hunger Tanzania, Zachary Imeje, anasema mwongozo huo si tu ahadi mpya ya kitaifa ya kuwafikia watoto walio hatarini zaidi kwa huduma bora, bali unawawezesha wahudumu wa afya kuwa mstari wa mbele, kuimarisha mifumo ya afya, na kumpa kila mtoto nafasi ya kustawi, bila kubaguliwa.
"Mwongozo huu mpya umeandaliwa ili kuchochea kasi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) Namba 2 na 3, kwa lengo la kumaliza njaa, kuboresha afya ya watoto, na kupunguza vifo vinavyotokana na utapiamlo," anasema Imeje.
Anasema mtindo wa baadhi ya kinamama kutonyonyesha mtoto kikamilifu una madhara makubwa, hasa ukondefu mkali na kwamba kupitia mwongozo huo na maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji, wanatarajia kuona mabadiliko.
"Sisi shirika la Action Against Hunger, tunaamini uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa mwaka 2025 wa kuzuia na kutokomeza utapiamlo mkali utakuja na matokeo chanya," anasema.
Imeje anasema mwongozo huo ni ahadi mpya ya kitaifa ya kuwafikia watoto walio hatarini zaidi kwa huduma bora, kwa wakati ufaao ili kuendelea kuhimiza akina mama umuhimu wa kunyonyesha.
MAENDELEO LISHE
Mwakilishi wa wadau wa maendeleo ya lishe, Joyce Ngegba, anasema wapo tayari kusaidia utekelezaji wa miongozo mipya, kuimarisha uwezo katika ngazi zote za mfumo wa afya na kuhimiza kuwapo kwa ufadhili endelevu, pamoja na kuendeleza ushirikiano baina ya sekta mbalimbali.
"Hivyo, kwa niaba ya wadau wa maendeleo ya lishe na UNICEF, niipongeze serikali kwa tukio hili muhimu, tutaendelea kushirikiana kwa karibu katika kubadilisha maisha ya watoto wote nchini," anasema Joyce.
Joyce anasema dhamira ya wadau hao ni kukuza unyonyeshaji na kukabiliana na utapiamlo mkali kwa watoto, si tu kama vipaumbele vya kiufundi, bali pia kama wajibu wa kimaadili.
Anasema uzinduzi huo unawakilisha hatua muhimu katika jitihada za kitaifa za kutokomeza utapiamlo miongoni mwa watoto, kwa kusaidia mikakati ya Tanzania na miongozo mipya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2023.
"Mwongozo huu unachukua nafasi ya toleo la mwaka 2018, na umeboreshwa kwa mtazamo wa kisasa, jumuishi, shirikishi na unaotegemea ushahidi wa kisayansi ili kutoa mwongozo thabiti wa kusaidia watoto walio katika hatari ya utapiamlo," anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED