Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amesema hakuna mgombea mwingine anayeweza kumkaribia Rais Samia Suluhu Hassan kwa uzoefu na uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.
Dk. Kikwete ametoa kauli hiyo leo katika uzinduzi wa kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 uliofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Parkers, Dar es Salaam, ambapo amesisitiza kuwa mafanikio makubwa ya Samia ndiyo yanayompa nafasi ya kipekee katika siasa za nchi.
Amesema tangu Rais Samia aingie madarakani, ameonesha ubunifu mkubwa akiwemo kubuni Falsafa ya R4 ambayo imesaidia kuimarisha amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
“Amepokea uongozi katikati ya janga la UVIKO-19 na kutuongoza vyema kiasi cha kupunguza madhara yake. Fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya janga hilo, badala ya kwenda kwenye ruzuku kwa kampuni za wafanyabiashara kama ilivyokuwa katika baadhi ya nchi za Afrika, yeye alizielekeza kwenye kuimarisha huduma za jamii ili wananchi wanufaike moja kwa moja,” amesema Kikwete.
Aidha, amesema Samia alipokea nchi ikiwa inatekeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, ambayo ilihitaji fedha nyingi huku baadhi yake zikiwa hazijatengewa bajeti.
“Miongoni mwa miradi hiyo ni Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, ujenzi wa Makao Makuu Dodoma, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Magufuli. Kwa uhodari wa Samia, miradi hii imekamilika na mingine inaendelea kwa kasi kuliko ilivyotarajiwa,” amesema Kikwete.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED