Wanaohamasisha kususia uchaguzi wanaipa nguvu CCM – Nondo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:48 AM Jul 02 2025


Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo.

Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, amesema kuwa watu wanaowahamasisha wananchi kutoshiriki kupiga kura wanakipa nguvu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa sababu hatua hiyo huongeza nafasi ya chama tawala kuendelea kulitawala bunge bila ushindani.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana Julai 1, 2025 katika eneo la Kalinzi, Jimbo la Kigoma Kaskazini, Nondo alisema:

“Unapowahamasisha watu wasishiriki uchaguzi, kwa maana nyingine unaipa CCM nguvu ya kulitawala Bunge bila upinzani wowote. Wanaoeneza wazo la kususia wanatumikia mfumo tunaoupinga.”


Mwenyekiti huyo wa vijana alisisitiza kuwa ACT Wazalendo haitokimbia uchaguzi, hata kama mchakato wa uchaguzi huo umejaa dosari. Alisema chama hicho kimeamua kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili “kuwanyang’anya wahuni silaha zao kwa kuingia ulingoni na kuwashinda.”

“Tunasema tunakwenda kwenye uchaguzi wa kihuni kuzuia uhuni. Kususa hakuzuii udhalimu, bali kunautengenezea nafasi,” aliongeza Nondo.


Hotuba hiyo imekuja wakati taifa likielekea katika uchaguzi mkuu unaotawaliwa na kauli mbiu tatu; Oktoba Linda Kura; ACT Wazalendo, No Reforms No Election; CHADEMA na Oktoba Tunatiki; CCM.

ACT Wazalendo kupitia viongozi wake wa vijana wameendelea kuhimiza ushiriki mpana wa wananchi katika zoezi la uchaguzi kama njia ya kweli ya kupambana na mfumo wa kimabavu.