Majaliwa abadili gia angani, watano wajitokeza kumrithi Ruangwa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:43 PM Jul 02 2025
Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mtandao
Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Makada watano wa CCM wamejitokeza kumrithi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika nafasi ya ubunge wa Ruangwa mkoani Lindi, kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Akizuzngumza na Nipashe Digital, Katibu wa CCM wa wilaya ya Ruangwa Abbas Mkweta, amesema hadi kufikia leo ni makada watano aliochukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Amekumbushia kuwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu lilianza Juni 26 na kwamba litahitimishwa leo majira ya saa kumi jioni na kwamba kama bado kuna kada anataka fomu afanye haraka.

"Wanachama hao ni Bakari Nampenya, Philip Makota, Fikiri Liganga, Hashim Mparuka na Kaspa Muya. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamua kupumzika na kuwaachia wengine," amesema Mkweta.

Hashim Mparuka.

Mketa amesema Waziri Mkuu amemwambia kuwa ameona apumzike ili makada wengine wa chama hicho wachukue kijiti waweze kuiendeleza Ruangwa na kwamba atakayeshinda atampa ushirikiano.


"Vilevile, amesema amewapa baraka vijana ili nao walitumikie taifa, lakini pia ameniachia ujumbe kwamba tuhakikishe Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Emmanuel Nchimbi na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi wanapata kura nyingi katika uchaguzi mkuu ujao," amesema.


Mmoja wa makada hao Hashim Mparuka ameiambia Nipashe Digital kuwa amechukua fomu hiyo leo na ataijaza na kuirejesha kabla ya saa kumi, kwa ajili ya kubeba mikoba ya Waziri Mkuu.

Juni 26 akiwa bungeni jijini Dodoma, akiwasilisha hotuba ya kuhitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa aliwashukuru wananchi wa Ruangwa kuendelea kumuunga mkono na kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Baada ya kuwashukuru katangaza kuwa atarejea tena kuwania ubunge katika jimbo hilo. Lakini ghafla amebadili uamuzi huo na kusema ameamua kukaa pembeni na kuwaachia vijana.

Hashim Mparuka.