Tax agusia nidhamu michezoni

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 05:08 PM Jul 02 2025
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Steregomena Tax
Picha: Mtandao
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Steregomena Tax

WANAMICHEZO wametakiwa kuwa na nidhamu katika mashindano mbalimbali, ili kuepusha migogoro ndani ya timu zao.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Steregomena Tax, wakati  kwenye ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup 2025), kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

"Ninaomba kila mchezaji azidishe nidhamu usipokuwa na nidhamu utasababisha migogoro ndani ya timu, amesema Dk. Tax.

Aidha amezipongeza kamati zote za mashindano kwa ubunifu mkubwa walioufanya na kuwataka watanzania kupenda michezo kwani hujenga afya. 

Amesema kupitia mashindano hayo watapatikana wachezaji watakaounda timu ya taifa ambayo itapata fursa ya kushiriki mashindano mbali mbali nje na ndani ya nchi. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Brigedia Jenerali Said Hamis Said, amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo pamoja na kudumisha mshikamano wa timu za majeshi.

"Mwaka huu tumeboresha mashindano haya kwa kiasi kikubwa kwa michezo mingine kuongezeka na kufikia idadi ya michezo 15, iliyoshirikisha wanaume na wanawake kutoka Kamandi mbalimbali za jeshi,” amesema Said. 

Ameitaja michezo itakayoshiriki kuwa ni mpira wa miguu, kurusha tufe, mpira wa wavu, kulenga shabaha, netiboli, kuogelea, ngumi, vikwazi, gofu, pamoja na mieleka. 

Amesema amewashukuru wadau pamoja na wadhamini mbali mbali kwa kuwaunga mkono na mashindano hayo kufanyika kwa weledi mkubwa, ambapo vitatumika viwanja mbalimbali vilivyopo  Dar es Salaam.