Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, wameweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara bila ya kupoteza mechi yoyote ya ugenini msimu huu, lakini kubwa zaidi ni kuvunja rekodi zake yenyewe.
Timu hiyo iliyocheza michezo 30, ikishinda 27, sare moja na kupoteza miwili, yote imepoteza ikicheza ikiwa nyumbani.
Kwa mujibu wa Kitengo cha Rekodi na Takwimu za Michezo cha Nipashe, Yanga imecheza michezo 15 ugenini, ikishinda 14 na kutoka sare moja tu.
Msimu huu, Yanga imebeba ubingwa ikivunja rekodi zake yenyewe, ikitwaa ubingwa ikiwa na pointi 82, wakati msimu uliopita ilimaliza na alama 80.
Imeshinda mechi 27 wakati msimu uliopita ilishinda michezo 26, ikipachika mabao 83, tofauti na msimu uliopita ilipofunga mabao 71.
Msimu huu imeruhusu mabao 10 tu wavuni mwake, msimu uliopita wavu wake ulitikiswa mara 14, ikipata sare moja, wakati msimu uliopita ilitoka sare mara mbili.
Michezo ambayo imeshinda ugenini ni dhidi ya Kagera Sugar, ikitoka na ushindi wa mabao 2-0, ikiichapa KenGold, Simba, Coastal Union na Singida Black Stars, zote ikishinda bao 1-0, kila mchezo, huku ikiibamiza Tabora United mabao 3-0.
Mechi zingine ilizoshinda ugenini ni dhidi ya Namungo, ikipata ushindi wa mabao 2-0, Dodoma Jiji na Fountain Gate, kila timu ikichapwa 4-0, KMC ikitwangwa 6-1, Pamba Jiji ikilazwa 3-0, Prisons na Mashujaa FC, kila timu ikilambwa 5-0.
Sare pekee iliyotoka ugenini ilikuwa ni dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyochezwa, Februari 10, mwaka huu, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Haikuwa sare pekee ugenini tu, bali ndiyo pekee ambayo Yanga msimu huu imeipata kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga imepoteza michezo miwili msimu huu ambayo yote ilikuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Ilikutana na kipigo cha bao 1-0, Novemba 2, mwaka jana, dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, siku tano baadaye, Novemba 7, mwaka jana, ikiwa kwenye uwanja huo huo, ilikutana na kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Tabora United.
Makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji, hakusita kuelekeza furaha yake kwa timu hiyo kutwaa ubingwa huku ikiweka rekodi nyingi.
"Tunastahili kujivunia, tumechukua mataji yote ya ndani msimu huu, na hii yote imesababishwa na nidhamu, kujitoa katika kuhakikisha unalitekeleza lile ambalo unaliamini na kulisimamia pasi ya kuyumba, kutoka kwenye njia ile ambayo unaona ni sahihi katika kulitekeleza lile ambalo unaona lina manufaa, hicho kimekuwa kikitusaidia sisi," alisema Arafat hapo jana.
"Tunataka sasa tujiandae na kujidhatiti ili kupata mafanikio kwenye anga za kimataifa."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED