Tanzania kuimarisha Hifadhi za Wanyamapori zinazovuka Mipaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:40 AM Jul 03 2025
Kamishna wa Polisi (CP.) Benedict Wakulyamba
Picha: Mwandishi Wetu
Kamishna wa Polisi (CP.) Benedict Wakulyamba

Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutekeleza mpango wa hifadhi na mifumo ikolojia inayovuka mipaka ya nchi mbili au zaidi ili kudhibiti ujangili, kulinda rasilimali na kukuza uchumi wa jamii kupitia utalii wa wanyamapori.

Akifungua kikao cha wataalam wa ndani jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kamishna wa Polisi (CP.) Benedict Wakulyamba amesema hatua hiyo itafungua shoroba za wanyamapori na kuongeza kipato kwa wananchi wanaoishi maeneo ya jirani. Alisisitiza kuwa matumizi endelevu ya maliasili kama asali na biashara ya kaboni yataimarika.

CP. Wakulyamba ameeleza maeneo muhimu ya ushirikiano kuwa ni pamoja na usimamizi wa pamoja wa mifumo ikolojia, wanyamapori, misitu na maji, pamoja na kuimarisha maendeleo ya kijamii kupitia fursa za utalii na biashara.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe, amesema kikao hicho kitapanga kuanzishwa kwa Hifadhi ya Pamoja (TFCA) kati ya Tanzania na Zambia na kubaini fursa zitakazochochea ustawi wa jamii. Ameongeza kuwa Tanzania tayari ina ushirikiano na Msumbiji katika mfumo wa Selous–Niassa tangu 2007.

Mpango huu mpya unatekeleza maazimio ya mkutano wa wakuu wa nchi za SADC uliofanyika Harare, Zimbabwe mwezi Mei 2025, yaliyolenga kuimarisha hifadhi zinazovuka mipaka kwa faida za kiuchumi na kiikolojia.