Mafanikio ya Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi, inaelezwa yamewagawa viongozi wa klabu hiyo ambapo awali walitaka kuachana naye na kuleta kocha mpya.
Hata hivyo, kutokana na kuiongoza timu hiyo kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu na Kombe la FA kume- wafanya baadhi ya viongozi kutaka aendelee kuifundisha timu hiyo msimu ujao.
Awali kulikuwa na tetesi Yanga ingeachana na kocha huyo aliyejiunga nayo wakati ligi ikiwa imeshaanza msimu huu.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, inaeleza uwezo aliouonyesha kocha huyo wapo wanaotamani aendelee kuiongoza timu msimu ujao kwenye ligi na mashindano ya kimataifa.
“Awali ilionekana kama angekuwa kocha wa muda, lakini ameonyesha uwezo mkubwa ameikuta timu tayari ipo kwenye mashindano akitokea Singida Black Stars, lakini ameweza kuhimiri presha na kuisaidia kutetea makombe yote, sasa wapo wanataka aendelee kuinoa timu msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Aidha, alisema uongozi utatoa taarifa yake hivi karibuni juu ya timu kuanzia benchi la ufundi na usajili utakaofanyika kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.
Kocha huyo alijiunga na Yanga Februari mwaka huu akitokea Singida Black Stars na ameiongoza Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Mechi yake ya kwanza kuisimamia timu hiyo ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania Februari 10 ambayo walitoka suluhu.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe (pichani), amesema timu hiyo itafanya usajili wenye tija kwa ajili ya kuongezea makali kikosi chao.
Alisema wanataka kuona wanafanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika lakini pia kutetea tena ubingwa wa mashindano ya ndani kwa miaka mitano mfululizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED