Siku chache baada ya kuthibitika kiungo Fabrice Ngoma anaondoka, Uongozi wa klabu ya Simba tayari umeanza mchakato wa kumpata mbadala wake ambapo taarifa zinaeleza wametua kwenye klabu ya Bravo do Maquiz.
Simba ipo kwenye mazungumzo na kiungo, Higino Epalanga Kapitango, ili kurithi kuchukua nafasi ya Ngoma.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba na vyanzo vingine vya nje, vinasema kumekuwa na mazungumzo ya siku kadhaa ili kupata saini ya mchezaji huyo ambaye alicheza michezo yote ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliomalizika akiwa na kikosi hicho, kilichokuwa kundi moja ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Chanzo kimeliambia gazeti hili kuwa viongozi wa klabu hiyo, wanamuona mchezaji huyo mwenye miaka 22, ndio mbadala sahihi wa Ngoma kwani anasifika kwa upigaji mzuri wa pasi, na kufunga mabao ya mbali.
“Hata kocha Fadlu, amemkubali kiungo huyo, halafu anacheza namba nyingi, ni fundi wa kuchezea mpira mguuni, ana uwezo wa kucheza kiungo wa chini, kiungo wa juu na winga, lakini pia hata namba 10, nyuma ya mshambuliaji.
“wenye mechi za Kombe la Shirikisho tulimuona akiwa anacheza namba tofauti tofauti, lakini Simba inataka kumtumia kama kiungo wa kati kwa sababu ya uwezo wake wa kupiga pasi zinazofika,” alisema mtoa taarifa wetu.
Mchezaji huyo aliingia kipindi cha pili kwenye mchezo kati y Simba dhidi ya Bravo do Maquis uliopigwa Novemba 27, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Ben- jamin Mkapa, Dar es Salaam na kuibadilisha kabisa timu hiyo kiuchezaji.
Katika mchezo wa mzunguko wa pili, uliopigwa, Januari 12, mwaka huu nchini Angola, mchezaji huyo alianza, mechi ikiisha kwa bao 1-1.
Mbali na mchezaji huyo, taarifa zinasema klabu ya Simba pia inafanya mazungumzo na kiungo mkabaji raia wa Ivory Coast, Serge Eric Zeze, ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na klabu ya Raja Casablanca.
Kwa sasa Simba ipo kwenye harakati za usajili wa wachezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwahi kuwasilisha majina Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Fadlu pia amewapa wachezaji wa Simba mapumziko ya wiki mbili tu, kabla ya kurejea kutengeneza kikosi tayari kwa msimu ujao.
Kocha huyo amewaaambia mabosi wa Simba kuwa anahitaji wachezaji wenye uzoefu, wenyeari ya kupambana na uwezo wa kukabiliana na michezo mikubwa.
“Simba sasa inahitaji wachezaji wenye ubora wa kuweza kukabiliana na michezo mikubwa, angalia tumeshindwa dhidi ya Yanga, pamoja na RS Barkane, tunahitaji kuwa na wachezaji bora zaidi ya hapa tulipo na wenye ari ya kupambana,” alisema Fadlu.
Simba imemaliza msimu huu pia bila kutwaa ubingwa wowote baada ya kuishuhudia Yanga wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED