Kampuni tatu zapata vibali tiketi mtandao

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 05:23 PM Jul 02 2025
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, LATRA, Salum Pazzy.
Picha: Imani Nathaniel
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, LATRA, Salum Pazzy.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza kuwa hadi Juni 30, 2025, kampuni tatu za mifumo ya tiketi mtandao—Ottap Agency, Hashtech Tanzania na Iyishe Company—ndizo pekee zilizokidhi vigezo na kuruhusiwa kutoa huduma kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, LATRA, Salum Pazzy, amesema kuwa  kampuni nyingine sita zimepewa siku 14 kukamilisha taratibu, zikiwemo AB Courier, Busbora na Logix, huku Duarani na Itule zikipewa siku saba (7) za matazamio kutokana na changamoto kubwa zaidi.

LATRA imesisitiza kuwa kampuni zisizotajwa hazitambuliki kisheria, na wasafirishaji wanashauriwa kutumia mifumo halali pekee ili kuepuka usumbufu. Aidha, mifumo yote inapaswa kuunganishwa na mfumo jumuishi wa LATRA (CeTS/UTS), unaopatikana kupitia tiketi.latra.go.tz kwa huduma za SGR, MGR na mabasi ya mikoani.