Koka arejea 'ulingoni', kutetea Jimbo la Kibaha Mjini

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:35 AM Jun 30 2025
Koka arejea 'ulingoni', kutetea Jimbo la Kibaha Mjini
Picha: Mpigapicha Wetu
Koka arejea 'ulingoni', kutetea Jimbo la Kibaha Mjini

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sylvestry Koka, amejitosa tena kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge kwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Koka amekabidhiwa fomu hiyo jana Juni 29, 2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Isack Kaleiya, katika ofisi za chama hicho.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, Koka alisema ameamua kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake ili aweze kuendelea kulitumikia Jimbo la Kibaha Mjini, ambalo aliliongoza kwa kipindi cha miaka 15.

“Natambua miongozo ya chama changu. Nikiteuliwa nitawajibika kumnadi mgombea wa Urais na mgombea mwenza, na hata kama sitateuliwa bado nitawajibika kuwanadi wagombea wengine. Nafahamu misingi yote ya chama na nimejiandaa kwa yote yanayokuja,” alisema Koka.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Isack Kaleiya, alisema mwamko wa wanachama kuchukua fomu umeongezeka kwa kasi, ambapo hadi sasa jumla ya watia nia 10, wakiwemo wanawake, wamejitokeza kuchukua fomu za ubunge.

Aliongeza kuwa kwa upande wa nafasi za Udiwani Viti Maalum, hadi sasa wanachama 22 wamechukua fomu, ambapo Juni 28 walikuwa 15 na Juni 29 wameongezeka 7.