NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema Tanzania, inatarajia kuzalisha umeme unaotokana na nyuklia utakaojumuishwa katika Gridi ya Taifa, ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme yanayotokana na ongezeko la viwanda.
Biteko amesema hayo leo, Juni 30, 2025, Kigali nchini Rwanda, wakati akihutubia katika mkutano kuhusu masuala ya nyuklia Afrika.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeiagiza Wizara ya Nishati chini ya uongozi wangu kuhakikisha kwamba hivi karibuni umeme utakayozalishwa unajumuishwa katika Gridi ya Taifa,” amesema Dk. Biteko.
Ametaja baadhi ya jitihada kuwa Juni, 2025, Tanzania iliandaa warsha, ili kutoa uelewa kwa wadau wa masuala ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi itakayoratibu na kusimamia shughuli za nyuklia.
“Serikali yangu itahakikisha inaendeleza mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia nyuklia kwa kutunga sera thabiti na kuanzisha mifumo ya sheria na udhibiti kwa ajili ya usimamizi wa raslimali ya nyuklia na uzalishaji wa umeme unaotokana na nyuklia, amesisitiza Dk. Biteko.
Vilevile amesema serikali itaongeza raslimali watu wenye ujuzi katika teknolojia za nyuklia, ili kutumia kikamilifu raslimali hiyo hususan katika maeneo mengine ikiwamo afya na kilimo.
Amesema tayari Tanzania ina nyaraka mbalimbali zinazoiangazia nyuklia kama raslimali ya msingi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya nishati ya baadae kama vile Sera ya Taifa ya Nishati, Mkakati wa Nishati Jadidifu na Sera ya Maendeleo ya Madini.
Hata hivyo amesema Serikali ina lengo la kuimarisha Sera ya Teknolojia ya Nyuklia ya mwaka 2013 ili kiakisi maendeleo ya hivi karibuni sambamba na kufuata viwango vya kimataifa.
Akifungua Mkutano huo Waziri Mkuu wa Rwanda, Dk. Edward Ngirente, amesema kuwa, ili kufikia Mpango wa Maendeleo wa Rwanda wa mwaka 2050 wa kuwa nchi ya kipato cha juu wanahitaji kuwa na uzalishaji wa umeme kwa kiasi kikubwa.
“Hivyo, Rwanda tumeamua kuzalisha umeme wa nyuklia kwa kuwa ni salama na wa uhakika na hauhitaji mvua ili kurahisisha maendeleo kwa kutumia teknolojia,” amesema Ngirente.
Waziri Mkuu wa Niger, Ali Mahamane Lamine Zeine, amesema kuwa nchi yake ina vyanzo vingi vya nishati ikiwemo maji na sasa imezindua mpango wake wa nyuklia hivyo nyuklia ni nishati safi na ina manufaa makubwa katika uzalishaji wa umeme barani Afrika.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mionzi ya Atomiki Rwanda, Dk. Lassina Zerbo, amesema kuwa Rwanda ipo katika hatua za mwishoni za kuanzisha vinu vya nyuklia vya kuzalisha umeme.
Mkutano huo unaofanyika kuanza Juni, 30 hadi Julai Mosi, 2025 nchini humo, unajumuisha wadau wa nishati kutoka ndani na nje ya Afrika wenye lengo la kuharakisha matumizi ya nyuklia kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ili kuleta mabadiliko ya nishati Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED