Jafo abainisha hatua kuondoa viwanda magofu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 05:07 PM Jun 30 2025
Waziri wa Viwanda na biashara Dk. Selamani Jafo
Picha: Christina Haule
Waziri wa Viwanda na biashara Dk. Selamani Jafo

WIZARA ya Viwanda na Biashara, imesema viwando vyote vilivyokufa na kugeuzwa magofu au magodauni nchini, vitarejeshwa mikononi mwa serikali, kwa ajili ya kuvifanyia marekebisho na kisha kuvitafutia wawekezaji, kukuza ajira na maendeleo ya viwanda.

Waziri wa Viwanda na biashara Dk. Selamani Jafo, amesema hayo leo, katika Mkutano wa Pili wa Wizara ya Viwanda na Biashara uliokutanisha washiriki 250, wakiwamo maaofisa biashara wa mikoa na wakuu wa idara ulioandaliwa na Wakala wa Usajili na Leseni (BRELA) na kwamba tayari wameanza utekelezaji katika mkoa wa Tanga.

Dk. Jafo anasema wizara itaendelea kupitia viwanda hivyo vikiwamo vya mkoa wa Morogoro, lengo likiwa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa lango la viwanda na biashara na kuwa na ajira za kutosha, huku ikizidi kukua kiuchumi.

Aidha anawaomba maofisa biashara kuanzisha mfumo wa kukusanya taarifa za viwanda viliyopo kila mkoa, ili kufanya maendeleo na kukua katika viwanda na ujenzi wa uchumi, kwa sekta ya viwanda nchi.

Jafo amewaomba maofisa biashara kusimamia mauzo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, sababu ni miongoni mwa mambo yanayofanya vizuri katika kuboresha biashara nchini.

Anasema kwa sasa Tanzania inasafirisha bidhaa mbalimbali nje ya nchi, ikiwamo Afrika ya Kusini hasa mchele.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Ntwale, amewataka wakuu wa idara kutambua kuwa wanajukumu la usimamizi na kuwaagiza kuimarisha mazingira ya kibiashara hususan kwa wafanyabiashara wadogo.

Ntwale amesisitiza uongozi mahiri utumike katika kuleta mipango madhubuti na ushirikiano, ili kuwa na mabadiliko yanayohitajika hasa ya kisekta ambayo yanapaswa kuingizwa kwenye mipango kupitia ilani mpya ilikayotolewa hivi karibuni.

Katibu Tawala Mkoa huo, Musa Musa, amehimiza ushirikiano kati ya wafanyabiashara na wakulima, ili kuleta muunganiko ambao unaonekana kutokuwapo kwa watu wa biashara na kilimo na kukwamisha utendaji wa kazi zao ambazo zinazofanana.

Mwenyekiti wa Bodi ya wizara hiyo, Prof. Neema Mori, amewataka wafanyabiashara kushirikiana na BRELA, kwa kutumia kauli mbiu zinazotolewa, ili kupiga hatua kwenye maendeleo kibiashara.