HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga, imevuka lengo la ukusanyaji mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2024/2025 na kukusanya Sh. bil 6.5.
Hayo yamebainishwa leo, Juni 30, 2025 na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Alexius Kagunze, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema katika mwaka huo wa fedha, walipanga kukusanya mapato ya ndani kiasi cha Sh. bil 6.4, lakini hadi kufikia Juni 27, 2025, wamevuka lengo na kukusanya Sh. bil6.5 sawa na asilimia 102.
"Tuna washukuru wananchi wa Shinyanga,kwa ulipaji wa mapato na ushuru kwa hiari yao, na kufanikisha kuvuka lengo la ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kupata Sh. bil 6.5," amesema Kagunze.
Amesema fedha hizo zitatumika katika matumizi mbalimbali ya miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo,umaliziaji ujenzi maboma ya zahanati, likiwamo la Mwamagunguli na uendeshaji wa shughuli za manispaa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED