RIPOTI MAALUM - 2 Chanzo mfumo dume kusimika mizizi bayana

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 02:51 PM Jun 30 2025
Mwandishi wa Nipashe, Neema Emmanuel, akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Machifu 
Tanzania (UMT), Aron Mikomanga, kuhusu namna mfumo dume unavyosababisha athari.....
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwandishi wa Nipashe, Neema Emmanuel, akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT), Aron Mikomanga, kuhusu namna mfumo dume unavyosababisha athari.....

SEHEMU ya kwanza ya ripoti hii maalum Jumapili iliyopita, ilieleza tatizo la mfumo dume na athari zake kwa jamii, wanawake na watoto. Sehemu hii ya mwisho inaonesha chanzo chake pamoja na suluhisho.

WADAU na wasomi wanaeleza chanzo kikuu cha tatizo la mfumo dume nchini kuendelea kushamiri ni pamoja na mila na desturi potofu zilizojengeka katika fikra za baadhi ya makabila kuwa mwanamume pekee ndiye mwenye uamuzi na anastahili kutafuta.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Dk. Dotto Bulendu, anasema tatizo hilo linaendelea kusimika mizizi kutokana na mila na desturi zilizopo.

Anasema mila na desturi nyingi nchini haziamini kuwa mwanamke anatakiwa kuongoza, akitoa mfano wa baadhi ya makabila ambayo yamekuwa hayawahusishi hata katika vikao vya uamuzi ndani ya familia na jamii.

Dk. Bilendu anasema asilimia kubwa husubiri kupewa taarifa na mrejesho wa majadiliano, huku akitaja hali hiyo kuwa imeathiri zaidi nafasi ya mwanamke katika jamii.

Anabainisha kuwa athari yake si tu katika jamii, imekwenda zaidi na kuathiri asilimia kubwa ya taasisi za elimu, vyuo, vyombo vya habari nchini na Afrika kwa ujumla.

“Katika maeneo hayo utagundua nafasi ya mwanamke katika uongozi ni ndogo na walioshika nafasi za uamuzi ni wanaume, japokuwa katika nafasi ya wakuu wa taasisi ya elimu wanaume ni wengi.

“Angalau kuna mabadiliko kidogo, usawa wa jinsia umechukua nafasi idadi ya wanawake inaanza kuongezeka katika uamuzi,” anasema Dk. Bulendu.

Anasema hata mwanamke akipata nafasi ya uongozi katika taasisi, bado jamii imejijenga katika mfumo kuwa siyo kiongozi na wanashindwa kutoa ushirikiano tofauti na akiongoza mwanaume, wengi wanachangia kuonesha mwanamke siyo kiongozi bora.

Kwa mujibu wa Dk. Bilendiu  hali hiyo imeathiri ufanisi wa wanawake katika utendaji kazi wao kutokana na kukutana na vikwazo vyingi wanapoongoza.

“Mimi ni Msukuma. Ikitokea  msiba wa mzee katika familia mnapokwenda katika vikao huko vijijini, wanawake huwa hawaitwi katika vikao vya ‘nzego’ (wanakijiji) kutoa maoni, bali wao wanaletewa taarifa,” anasema.

Anasema  kuna baadhi ya watu pia wanabeba tamaduni hizo na kuzihamishia kazini, hivyo kuwa kikwazo kikubwa katika usawa wa kijinsia na kusababisha mfumo dume kuzidi kushamiri.

Anataja tatizo katika tasnia ya habari na kuwa nafasi ya mwanamke katika kada ya mawasiliano nchini iko kwa asilimia 20, huku wanaume kwa muda mrefu wakitawala eneo.

Ofisa Mradi wa Usawa kwa wanawake wafanyakazi wa nyumbani kutoka Shirika la WoteSawa, Demitila Faustine, anasema mila na desturi zenye upendeleo wa kijinsia zikimweka mwanamke katika nafasi ya chini na kumpa mwanamume mamlaka zaidi, ndiyo sababu ya hali hiyo kuendelea kushamiri.

Anasema wanawake, hasa katika maeneo ya vijijini, mara nyingi hukosa fursa sawa za elimu na ajira zenye staha, jambo linaloendeleza utegemezi wao kwa wanaume na kuongeza uwezekano wa kunyanyaswa.

Faustine anasema licha ya kuwapo kwa sheria na sera zinazohimiza usawa wa kijinsia, utekelezaji wake mara nyingi ni dhaifu ikisukumwa na zaidi na mianya inayoruhusu ubaguzi kuendelea.

“Mfano, sheria za kazi hazitekelezwi kikamilifu kwa wafanyakazi wa majumbani, ambapo  baadhi ya jamii bado zinaamini kuwa unyanyasaji wa kijinsia ni jambo la kawaida au ni suala la kifamilia ambalo halipaswi kuingiliwa na hivyo kutoa nafasi kwa mfumo dume kuendelea kustawi,” anasema.

Anasema wanatambua umuhimu wa kuwashirikisha wanaume na wavulana katika mapambano dhidi ya mfumo dume kupitia mikakati yao mbalimbali ikiwamo kuwaalika kushiriki katika warsha na mijadala inayojadili faida za usawa wa kijinsia.

Kuelimisha kuhusu majukumu ya kijinsia na jinsi mfumo dume unavyowaathiri pia kwa kuwabebesha mizigo isiyo ya lazima, sambamba na kutumia mifano chanya ya wanaume ambao wanashiriki kikamilifu katika majukumu ya kifamilia na kuheshimu wanawake.

Mchungaji wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Julia Gabriel.
CHIFU ANG’AKA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT), Aron Mikomanga, maarufu kama Chifu Nyamironda wa Tatu, licha ya kukiri kuhusu kushamiri kwa tatizo la mfumo dume nchini, anataja hali hiyo kuwa ni sehemu ya mambo yaliyoundwa na viongozi wa kale kwa malengo binafsi.

Anasema ziko baadhi ya mila zimepitwa na wakati ikiwa ni pamoja na  hizo hivyo kuitaka jamii kuacha kuzishikilia kwa kisingizio cha utamaduni wa kimakabila.

“Baadhi ya mila hizo ziliwekwa na wazee kwa malengo yao maalum kwa kuona kwamba labda mwanamke hana kazi nyingine zaidi ya kuzaa na kulea watoto na kutunza familia, hivyo kumwondolea majukumu mengine lakini kwa sasa hali ni tofauti,” anasema.

Anasema wakati mwingine jamii inatafuta visingizio vya kukandamiza mwanamke  kwa kisingizio cha mila na desturi na kusahau kuwa zipo zilizowekwa kulingana na mazingira na sasa muda wake umeisha.

“Kwa kipindi hicho cha ujima wazee na jamii ilikuwa ni yawafugaji na wawindaji tu ambako jukumu la wanawake lilikuwa ni kukaa nyumbani, na baba alikuwa anaondoka kwa muda mrefu kutoka hapo labda ndipo wakachukulia kuwa mama ni wakukaa nyumbani bila majukumu si kweli,” anasisitiza.

Anasema akiwa kiongozi wa kimila, ameliona hilo linaweza kuwa tatizo na kuchangia watoto wa kike wasiweze kupata haki zao kulingana na elimu na vipawa walivyonavyo, hivyo kupinga huo mtazamo na kuiomba serikali na jamii ielewe kuwa kila jambo linaende na wakati wake hivyo mwanamke apewe mazingira wezeshi.

“Hata viongozi wa mila na desturi wanaheshimu utu, haki ya mwanamke, kipawa na kipaji alichopewa na mwenyezi Mungu, hivyo asihesabike kuwa mwanamke anayo kazi moja katika jamii kuzaa na kulea familia.

“Anapaswa kutumia kipawa chake na karama yake ambayo ni elimu, nguvu na uwezo na utashi kwa manufaa yake na jamii na taifa kwa ujumla,” anasema.

NINI KIFANYIKE

Dk. Dotto Bulendu anataja mbinu pekee ya kukabiliana nalo kuwa ni kutoa elimu na kufanya kampeni kubwa kwa wanaume na vijana ili kuwabadilisha mitazamo yao watambue kuwa siyo mwanamume tu anatakiwa kuwa kiongozi na kufanya kazi.

Mbali na kuwataka wanafunzi vyuoni kutoendekeza mila na desturi potofu, anashauri elimu kuendelea kutolewa zaidi hasa katika taasisi za elimu, vyuo vya kati na vyuo vikuu ili kuwa na kizazi kinachothamini usawa wa kijinsia.

Msaikolojia Tiba kutoka Somedics Polyclinic Health Centre, Saldin Kimangale, anasema athari za kisaikolojia kwa wanawake inachangia kuongezeka kwa hatari ya matatizo ya afya ya akili kama vile wasiwasi wa muda mrefu.

Anataja athari nyingine ni sonona, kupoteza kujiamini, kuchoka kihisia na kukosa uthubutu wa kufikia malengo binafsi, kukubali kupimwa kwa kigezo cha maumbile badala ya uwezo binafsi.

 “Kuwa na sera za kusimamia uadilifu zaidi wa kijinsia, kuweka mazingira rafiki kwa jamii kuanzia ngazi ya familia, kutoa fursa sawa za kiuchumi, huduma na msaada wa kisheria kwa waathirika na kuendesha kampeni za elimu juu ya hali hii kupitia majukwaa mbalimbali na mitandao ya kijamii ni miongoni mwa njia zinazoweza kutokomeza tatizo hili,” anasema.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, Julia Gabriel, anasema mfumo dume ni tatizo kubwa kwa sasa kutokana na kuwa wanawake wengi wameacha kazi kwa ajili ya kulinda amani ya ndoa zao.

Anasema ukweli maisha yao yanabadilika na kuwa ya tabu akitaja kesi iliyoko mikononi mwake kuwa mwanamume alimwachisha kazi mke wake ambaye amesoma mpaka Shahada ya Uzamili ‘Masters’ akapata kazi serikalini.

Mchungaji Gabriel anasema mume wake anakiwango hichohicho cha elimu na alikuwa na kazi, lakini alipata shida kazini kwake akaachishwa.

Anaeleza kuwa mara baada ya kuachishwa kazi aliendelea kuisimamia miradi waliokuwa wamewekeza.

Anasema mume wake baada ya kuona mke wake anaendelea kufanya kazi na kupata ofa mbalimbali za kwenda mpaka nje ya nchi, alimtaka aache kazi ili awe mama wa nyumbani.

“Akimwambia akisafiri kikazi kwenda sehemu yoyote atakutana na talaka mlangoni, hivyo ilimlazimu kuacha kazi.

“Hii ni kesi mbichi kabisa huyu mama alichukua uamuzi wa kuandika barua ya kuacha kazi ndani ya saa 24 kisa mwanamke alienda nyumbani akiwa na furaha huku amebeba na barua ya kupandishwa cheo.

“Mwanamume aliipokea barua hiyo pasipokuwa na furaha huku akimwambia ‘sikia mimi ni mwanaume humu ndani hiyo nafasi yako iishie mlangoni’ akijua analinda ndoa kumbe alijidanganya kwa sasa mwanaume ana uhusiano na wanawake wengi yeye akibaki tu nyumbani akiwa hana cha kufanya na maisha magumu,”anasema.

Mchungaji Gabriel anasema kama mchungaji anapokea kesi nyingi zikiwamo za watu ambao wanajuta kuacha kazi kwa sababu ya kulinda heshima zao na kusikiliza takwa la waume zao.

“Nakumbuka niliwahi kuunda kundi la WhatsApp kwa ajili ya kuwajenga na kuwaelimisha wanawake namna bora ya kuishi lengo langu lilikuwa jema, siku moja niliwakutanisha wote 350 ufukweni walibadilishana mawazo.

“Lakini baada ya tukio hilo, nilipokea simu kutoka kwa Askofu akiniambia anasikia kuna harakati ninaendelea nayo kwa madai kuwa ninataka kuharibu ndoa za wanawake hapo.

“Wanaume walianza kuleta taharuki, wakati lengo langu lilikuwa kujenga wanawake wasimamie nafasi zao ili waweze kulinda ndoa zao ipasavyo, hivyo hizo ni changamoto pia katika kulisimamia hili,” anasema.

Anashauri jamii kuwajengea uwezo wa kujiamini na kujisimamia mtoto wa kike na wa kiume tangu akiwa mdogo, huku kanisa nalo liwajengee uwezo viongozi wa dini kama kundi lenye ushawishi mkubwa katika jamii.