Marekani yavutiwa na Bandari Mtwara

By Baraka Jamali , Nipashe
Published at 06:02 PM Jun 30 2025
Marekani yavutiwa na Bandari Mtwara
Picha: Baraka Jamali
Marekani yavutiwa na Bandari Mtwara

KAIMU Balozi wa Marekani nchini, Andrew Lentz, ameeleza dhamira ya nchi yake kushirikiana na Tanzania katika kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha bidhaa kwenda masoko ya kimataifa.

Ziara hiyo imekuja wakati Tanzania inaendelea kuimarika kimkakati katika sekta ya miundombinu ya usafirishaji.

Katika ziara hiyo, leo, Juni 30, 2025, Balozi Lentz ametembelea Bandari ya Mtwara na kujionea maendeleo yaliyofanyika, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa gati jipya lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa na shehena nyingi zaidi. 

Ameeleza kuridhishwa na maboresho hayo, akisisitiza kuwa mazingira hayo mazuri ya biashara yanaweza kufungua milango kwa makampuni ya Marekani kuwekeza na kutumia bandari hiyo kama lango la kibiashara kwa ukanda wa Kusini mwa Tanzania na nchi jirani.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amempongeza Rais wa Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa anazozifanya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuvutia wawekezaji wa kigeni. 

Marekani yavutiwa na Bandari Mtwara
Amebainisha kuwa ziara ya balozi huyo ni matokeo ya diplomasia makini ya uchumi inayoongozwa na serikali ya awamu ya sita.

“Uwapo wa Balozi Lentz, Mtwara, ni ishara ya imani waliyonayo wawekezaji wa kimataifa kwa mazingira ya biashara ya Tanzania. Tutaendelea kuboresha miundombinu na kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuhakikisha fursa hizi zinaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wetu,” amesema Kanali Sawala.

Marekani yavutiwa na Bandari Mtwara
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ulianzishwa rasmi mwaka 1961 mara baada ya Tanganyika kupata uhuru. Tangu wakati huo, nchi hizi mbili zimekuwa na ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwamo elimu, afya, usalama, na hivi sasa biashara na uwekezaji ukichukua nafasi ya juu katika ajenda za pamoja.

Ziara ya Kaimu Balozi Lentz inaashiria nia ya Marekani kuimarisha zaidi ushirikiano huo kupitia uwekezaji wa moja kwa moja, huku Bandari ya Mtwara ikitajwa kuwa kitovu muhimu cha kuunganisha biashara baina ya mataifa hayo na maeneo mengine ya Afrika Mashariki na Kusini.