Serikali imesambaza kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza (Gereza la Ukonga) mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko yake 464 ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama njia ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia nchini ambapo msisitizo ni angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ifikapo Mwaka 2034.
Hafla ya ugawaji wa mitungi na majiko yake iliongozwa na Balozi, Radhia Msuya, Mkurugenzi wa Bodi ya Nishati Vjijini (REB) katika gereza la ukonga, Jijini, Dar es Salaam, leo Juni 30, 2025 ambapo kwa upande wa Magereza uliwakilishwa na Msaidizi wa Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi, (ACP); Athuman Recha.
Balozi, Radhia amesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Watumishi hao watasambaziwa mitungi ya gesi na majiko yapatayo 464 na kuongeza kuwa huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kama nyenzo ya kulinda afya za Watanzania, kulinda na kutunza mazingira
Amesema kuwa, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia makubaliano na Jeshi la Magereza ili kuwawezesha, kuhama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama kwenda katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika magereza yote nchini.
“Serikali kupitia REA, ilishaanza uwezeshaji kwa Jeshi la Magereza na wameshaanza kutumia Nishati Safi na kwa msisitizo huo, tuliona ni vyema, kuwawezesha Watumishi na Maafisa ili nao waachane na nishati chafu ili kulinda afya zao pamoja na kulinda mazingira yetu”. amesema, Balozi, Radhia.
Naye, Mkurugenzi wa Fedha na Uwezeshaji, CPA, Daniel Mungure ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), amewataka watumishi wa jeshi la magereza kuibeba Ajenda ya Rais Samia ya kuwa Mabalozi wa Nishati Safi ya kupikia kwa kuendelea kutumia gesi na siyo kuni na mkaa.
Akishukuru kwa uwezeshaji huo kwa Watumishi na Maafisa wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Mwandamizi, (SSP); Moses Mumbi amesema, wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajali na kuongeza kuwa teknolojia hizo za Nishati Safi ya Kupikia si tu zinalinda afya zao lakini zinaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wa kuwahudumia Mahabusu na Wafungwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED