Serikali yabeba gharama za maziko, 39 waliofariki ajalini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 04:02 PM Jun 30 2025
Ajali ya Same.
Picha: Mtandao
Ajali ya Same.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema serikali imeamua kubeba gharama za maziko ya watu 39, waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la saba saba, nje kidogo ya Mji wa Same, baada ya mabasi mawili ya abiria kugongana uso kwa uso na kutetetea kwa moto.

Akizungumza leo, Juni 30, 2025, Babu amesema wananchi hao waliopoteza maisha watasitiriwa kwa heshima zote.

“Kwa hiyo leo kamati ya maafa, ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, inakuja ili tuweze kukaa, tufanye hiyo tathimini ya mwisho na tuweze kuwahudumia hawa katika shughuli hizi za mazishi baada ya wao kufika.

“Hatuwezi kuwazika pamoja maana yake vinasaba vikija watachukua miili. Tumefanya kubandika alama katika kila mwili wa marehemu halafu tutakabidhi kwa ndugu. 

Kwa hiyo hapo sasa, serikali ndo itaingia kwa maana ya kusaidia sasa usafiri na Jumatano tutoa majibu ya DNA na Alhamisi tutawakabidhi miili kwa ajili ya maziko.” 

Ajali hiyo iliyotokea jioni ya Juni 28 mwaka huu, iliyahusisha Basi la Kampuni ya Chanel One, lenye namba za usajili T 179 CWL, na basi dogo la abiia aina ya Toyota Coaster, namba T 199 EFX.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro (SACP), Simon Maigwa, amesema chanzo cha ajali hiyo, ni basi la Kampuni ya Chanel One aina ya Fusso, kupasuka tairi la mbele upande wa kulia na dereva kushindwa kulimudu na kuhamia upande wa kulia wa barabara na kugongana uso kwa uso na na basi hilo dogo. 

Miili 33 ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC na miili mitano imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same.