Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kuwa uamuzi wa baadhi ya vyama kususia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni sawa na kuipa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ushindi wa bure, hali itakayochangia kupatikana kwa viongozi wasiojali maslahi ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, wakati akihutubia wananchi wa Shinyanga katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Town.
Dorothy amesema ACT-Wazalendo imejipanga kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na kwamba haina mpango wa kususia, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuikabidhi CCM ushindi wa bila kupingwa. “Tutasimama kidete kulinda na kutetea demokrasia ya nchi yetu kwa kushiriki uchaguzi na kuwasimamisha wagombea wenye sifa watakaotanguliza maslahi ya wananchi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo, ameeleza kuwa wapo wanaosusia uchaguzi kwa makusudi au pengine kwa kushawishiwa, jambo linaloipatia CCM nafasi ya kuendelea kutawala bila ushindani. Amesisitiza kuwa tabia ya kususia uchaguzi inawadhuru wananchi moja kwa moja kwa kuwa hukosa fursa ya kupata viongozi wanaowatetea.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, amewahimiza wananchi wa Shinyanga kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi kwa kuchagua viongozi wenye dhamira ya kweli ya kubadili maisha yao kupitia matumizi bora ya rasilimali, hasa madini.
Naye Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA wa chama hicho, Emmanuel Ntobi, amesema ACT-Wazalendo haikubaliani na kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja kwa kisingizio cha kususia uchaguzi. Ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki uchaguzi ili kuendeleza mapambano ya kisiasa kwa njia za kidemokrasia.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Shinyanga, Hassan Ibrahimu, amewataka wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi na kulinda kura zao mara baada ya kupiga kura mwezi Oktoba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED