Tanzania sasa inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la kahawa, ikiwa imezipita nchi zilizokuwa vinara kama Kenya na Ivory Coast, katika hatua inayoashiria mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo.
Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dk. Stephen Nindi, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 15 wa Bodi ya Kahawa nchini uliofanyika jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Kilimo.
Dk. Nindi amesema Serikali itaendelea kutafuta masoko mapya ya kahawa ndani na nje ya Afrika ili kuinua kipato cha wakulima wa kahawa nchini na kuongeza mapato ya taifa kupitia mauzo ya zao hilo. “Lengo letu ni kuona kahawa ya Tanzania inakuwa na soko la uhakika kimataifa na inatumika katika maeneo mbalimbali duniani,” amesema.
Ameviagiza vyama vya ushirika kushirikiana na Bodi ya Kahawa katika kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili kuimarisha uzalishaji na ubora wa kahawa ya Tanzania. Vilevile, ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuhakikisha kahawa inachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa nchini, Primus Kimaryo, amesema Bodi inaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha kilimo cha kahawa, ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji katika maeneo mbalimbali.
Kimaryo amesema Bodi hiyo ililenga kufikia uzalishaji wa tani 300,000 za kahawa ndani ya miaka mitano, ingawa bado hawajafikia lengo hilo. Hata hivyo, ameongeza kuwa wanaendelea kujipanga upya kuhakikisha lengo hilo linafikiwa kwa ufanisi zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED