Rais Samia Suluhu Hassan amesema lugha ya Kiswahili ni urithi kwa Watanzania ambao unaweza kuchochea maendeleo.
Rais Samia amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Umoja wa Visiwa vya Comoro yaliyofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni jana.
Alisema eneo la Kusini mwa Afrika limegawanywa kuendana na lugha za watawala wa kikoloni na kuna mataifa yanazungumza Kiingereza, Kifaransa na wengine Kireno lakini Kiswahili ni lugha ya Kiafrika inayoweza kuunganisha mataifa hayo.
Ameomba Kiswahili kifundishwe shuleni na kitambulike nchini Comoro ili kujenga na kuimarisha umoja uliopo kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Alisema Tanzania ipo tayari kusaidia kutoa walimu na vifaa vya kufundishia ili kufanikisha hilo na akasema Kiswahili ni urithi wa pamoja wa mataifa hayo.
“Tukumbuke kwamba Kiswahili ni urithi wetu wa pamoja na ni daraja la maendeleo baina yetu,” alisema Rais Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED