Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema Mwenge wa Uhuru umekimbizwa jumla ya kilomita 895 na kukagua miradi 52 yenye thamani ya Shilingi bilioni 84, huku miradi yote ikiridhishwa na kukidhi vigezo vya utekelezaji.
Akizungumza Julai 5, 2025, wakati wa kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Arusha katika kijiji cha Kingori, kata ya Malula, wilaya ya Arumeru, Babu alisema mkoa wake umeonyesha mafanikio makubwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Babu, kati ya miradi hiyo, 22 ilizinduliwa rasmi, 20 iliwekwa mawe ya msingi na 10 ilitembelewa na kukaguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru. Alisema pia Mwenge huo ulitembelea miradi tisa ya kijamii inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya wawekezaji binafsi na Serikali, ikiwa ni ishara ya mshikamano katika maendeleo.
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mkoa huo umewagawia wananchi mitungi ya gesi 370 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 18.4, kama mbadala wa matumizi ya kuni na mkaa.
Katika sekta ya afya, Babu alisema ndani ya siku saba za mbio hizo, watu 1,801 walipima VVU na 12 walikutwa na maambukizi sawa na asilimia 0.67. Aidha, damu salama iliyopatikana ilikuwa unit 177, huku watu 812 waliopima malaria hawakubainika kuwa na ugonjwa huo.
Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, alisema elimu ilitolewa kwa wananchi, ambapo jumla ya kesi 401 ziliripotiwa, na kati ya hizo, 201 zilionyesha viashiria vya rushwa huku kesi 20 zikitolewa hukumu.
Kwa upande wa dawa za kulevya, jumla ya watuhumiwa 555 walikamatwa, zikiwemo kesi 232 zilizofunguliwa mahakamani, ambapo 106 zimeshatolewa hukumu.
Akihitimisha Mbio za Mwenge Mkoa wa Kilimanjaro, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ally Ussi, alisifu ubunifu, ufanisi na thamani ya miradi iliyotekelezwa. Alitoa pongezi kwa wakuu wote wa wilaya wa mkoa huo kwa usimamizi bora wa shughuli za maendeleo.
“Ningeshauri viongozi hawa wasiondolewe, waendelee kumsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwaletea wananchi maendeleo, kwani utendaji wao ni wa mfano,” alisema Ussi.
Ussi pia alimsifu Mratibu wa Mwenge Kimkoa, Irine Kiatu, na timu yake akiwemo Ashumu Marari kwa maandalizi bora na ushirikiano mzuri uliowezesha mafanikio ya mbio hizo. Aliahidi kuwa atamuomba Rais Samia awape vyeti waratibu 10 bora kitaifa ifikapo Oktoba 14.
Akitoa shukrani kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Ussi alimpongeza ASP Frank Agapiti na kikosi chake kwa ulinzi madhubuti wa Mwenge huo na kumuomba RPC kuwapa mapumziko ya siku sita hadi saba kama sehemu ya kutambua kazi yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED