BAADA ya kutangaza rasmi kumsajili beki wa kati, Lameck Lawi, klabu ya Azam FC, imetajwa kuwa ipo kwenye mazungumzo ya kuhitaji huduma ya kiungo wa KMC na timu ya taifa ya Tanzania, Ahmed Bakari 'Pipino', ambaye alitamba kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Kusini mwa Afrika (COSAFA), iliyomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kuwa maslahi ya mchezaji huyo yamefikiwa na amekubali kutua kwenye viunga vya Chamazi, kilichobaki sasa ni klabu hizo mbili kukubaliana, ili dili hilo liweze kukamilika.
"Ni mchezaji mzuri sana, ni kijana mdogo mwenye kipaji, tulimuona nchini Afrika Kusini kwenye michuano ya COSAFA, amechaguliwa tena kwenye kikosi cha timu ya taifa cha CHAN, tunadhani ataisaidia sana timu yetu kwenye kiungo cha kati pale," alisema mtoa taarifa.
Jopo la wataalam lilimchagua kiungo huyo mkabaji kuwa mchezaji bora ambapo alionesha kiwango cha hali ya juu na kuwazima kabisa viungo wa Eswatini, katika mchezo wa COSAFA, uliochezwa, Juni 11,Uwanja wa Free State, mjini Bloemfontein, Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Alichangia kwa kiasi kikubwa kuwaweka Stars mchezoni kutoka nyuma kwa bao moja, hadi kupata ushindi wa mabao 2-1, baada ya dakika 90.
Hata hivyo pamoja na ushindi huo, Stars ilitolewa kwenye michuano hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Kundi C, huku Pipino akibaki kuwa mchezaji pekee wa Tanzania kupata tuzo kwenye michuano hiyo msimu huu.
Akiwa na miaka 20, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu na kikosi cha timu ya wakubwa, akiwa amepandishwa na kikosi cha KMC, ambapo kwa sasa ameitwa kwenye kikosi kitakachocheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Amewahi kupitia kwenye Academy ya Celta Vigo ya Hispania, kabla ya kurejea nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED