Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Romanus Mapunda, ametangaza azma yake ya kugombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Mapunda, ambaye ni mkazi wa Kawe, Dar es Salaam, alitoa tamko hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Heritage Cottage, iliyopo katika Manispaa ya Songea.
Akiwa na ari kubwa, Mapunda alisema hana sababu yoyote ya kutogombea nafasi hiyo na kwamba amejipanga kikamilifu kushiriki mchakato wa kuwania urais kupitia CHADEMA, akisubiri taratibu rasmi za chama.
"Nimeamua kutangaza wazi kuwa nitachukua fomu ya kugombea urais kupitia tiketi ya CHADEMA. Naomba ushirikiano kutoka kwa chama changu kwa sababu nina mpango wa kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo nchini. Nataka kuijenga Tanzania mpya yenye mwelekeo mzuri kwa wananchi," alisema Mapunda.
Katika mkutano huo, Mapunda alimtaka Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antipas Lissu, kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu kauli mbiu ya chama cha "No Reform, No Election", akieleza kuwa imekuwa ikileta mkanganyiko miongoni mwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
"Kauli mbiu hii inaleta mkanganyiko mkubwa kwa sababu inaweza kutumiwa vibaya na kupotosha jamii. Ni muhimu kwa viongozi wa chama kutoa ufafanuzi wa malengo yake ili isizue taharuki miongoni mwa wanachama," alisisitiza Mapunda.
Mapunda pia aliwataka wanachama wa CHADEMA kuacha siasa za upinzani zisizo na msingi, akisema kuwa upinzani haumaanishi kupinga kila jambo bila sababu.
"Wanachama wa CHADEMA wanapaswa kuwa na mtazamo chanya. Siasa za upinzani si kupinga kila jambo kwa sababu tu limetolewa na chama kingine. Maendeleo hayana chama; yanaweza kutoka popote pale," alisema.
Katika hali isiyotarajiwa, Mapunda alimpongeza Diwani wa Kata ya Mshangano, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samwel Mbano, kwa juhudi zake za kusukuma maendeleo kwa wananchi wa kata hiyo.
"Diwani Mbano ni mfano mzuri wa kiongozi anayejituma kwa maendeleo ya wananchi. Ameshughulikia ujenzi wa shule za msingi na sekondari, upatikanaji wa maji safi na salama, umeme, huduma za afya kwa kujenga zahanati na kituo cha afya, pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya kata yake," alisema Mapunda.
Kwa mujibu wa Mapunda, viongozi wa aina hiyo wanapaswa kuigwa bila kujali chama wanachotoka, kwani maendeleo hayana chama na yanapaswa kuwa kipaumbele kwa viongozi wote wa siasa nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED