TANAPA yaagiza askari wake kulinda chanzo Mto Ruaha

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 02:02 PM Jul 03 2025
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Musa Kuji
Picha: Nebart Msokwa
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Musa Kuji

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Musa Kuji, amewataka maofisa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, waliopo Bonde la Ihefu wilayani Mbarali, mkoani Mbeya kuilinda ardhi oevu ya bonde hilo, ambalo ni chanzo kikuu cha Mto Ruaha.

Ametoa agizo hilo kwenye kikao kazi na makamanda wa Jeshi la Uhifadhi wa Vituo vya Doria vya Ikoga, Tagawano, Magda, Ulanga, Kiwale na  Ukwaheri, vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini.

Mto Ruaha unatajwa kuwa chanzo muhimu cha nishati nchini
Amefanya kikao na maofisa hao kwenye Ofisi za TANAPA Kanda ya Kusini, zilizopo Rujewa, wilayani Mbarali na amesema bonde hilo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa ikiwemo ustawi wa viumbehai vilivyomo ndani ya hifadhi ya Ruaha pamoja na uzalishaji wa umeme kwenye mabwawa ya Mtera, Kidatu na Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Maofisa na maaskari wa TANAPA wamepewa jukumu la kulinda hifadhi

"Mto Ruaha Mkuu umeendelea kuwa muhimu sana kwa taifa kwa sababu asilimia 60 ya maji yake ni muhimu kwa uhai wa mimeana wanyamapori ndani ya hifadhi yetu ambayo ni muhimu sana,” amesema Kamishna Kuji.


Kamishna Kuji yupo kwenye ziara ya kutembelea hifadhi zote nchini kwa lengo la kufanya mazungumzo na maofisa pamoja na askari, ili kuimarisha ulinzi wa hifadhi hizo, kukuza utalii na kuimarisha ushirikiano na jamii.