Wanaochangia damu hupunguza hatari ya saratani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:28 PM Mar 13 2025
Wanaochangia damu hupunguza hatari ya saratani
Picha; Mtandao
Wanaochangia damu hupunguza hatari ya saratani

WATU wanaochangia damu mara kwa mara, wana uwezekano mkubwa wa kuwa na mabadiliko ya (jeni) vinasaba katika damu yao, mabadiliko ambayo yanaweza kupunguza hatari ya kupata saratani, unaeleza utafiti.

Watafiti kutoka Taasisi ya Francis Crick, wanasema matokeo hayo yanavutia na yanaweza kusaidia kuelewa kwa nini saratani ya damu huibuka.

Utafiti wao ulilinganisha damu ya makundi mawili ya wanaume wenye afya njema walio katika miaka yao ya 60 – kundi la kwanza lilikuwa ni la wale waliochangia damu mara tatu kwa mwaka kwa miaka 40, kundi jingine ni wale waliochangia damu mara tano katika maisha yao.

Mabadiliko ya vinasaba ambayo hupunguza hatari ya kupata saratani ya damu yalikuwepo katika makundi ya watu hao walio changia damu. Lakini kwa sababu watu wenye afya bora ndio wanao changia damu, matokeo hayo bado hayatoi picha kamili.

Kadiri mtu anavyozeeka, seli za mwili - ikiwa ni pamoja na za damu - kawaida hubadilika, na hilo huongeza hatari ya magonjwa kama vile saratani.

Lakini watu wanapochangia damu, seli zilizopo kwenye uboho (ndani ya mifupa) hutengeneza seli mpya za damu ili kuziba pengo la damu iliyopotea – mchakato huo unaweza kusababisha mabadiliko ya maumbile ya vinasaba katika uboho.

Watafiti waligundua kiwango cha mabadiliko ya vinasaba katika damu ya kundi la watu 217, waliochangia damu mara kwa mara na kundi la pili la watu 212 waliochangia damu mara tano tu katika maisha yao.

Lakini mabadiliko hayo katika seli za uboho yalikuwa tofauti: 50% ni kwa waliochangia damu mara kwa mara. 30% kwa waliochangia damu mara chache.

"Ni aina ya mabadiliko ambayo hupunguza hatari ya kupata sarakani ya damu (leukemia)," anasema mtafiti wa utafiti huo Dk. Hector Huerga Encabo.

Na panya walipodungwa chembechembe hizi za seli za damu ya binadamu kwenye maabara, seli hizo zilionekana kufanya kazi vyema katika kutengeneza seli nyekundu za damu, anasema Dk Encabo.

BBC