Wazee nyumba za bandari Kurasini walalamikia eneo lao la wazi kumegwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:41 PM Mar 13 2025
Wazee nyumba za bandari Kurasini walalamikia eneo lao la wazi kumegwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Wazee nyumba za bandari Kurasini walalamikia eneo lao la wazi kumegwa

WAZEE walioliokuwa Askari Polisi wa Mamlaka ya Bandari(TPA), wamelalamika kuvamiwa kwa eneo lao la wazi lililopo Mtaa wa Minazini, Kata ya Kurasini wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na kujengwa oOfisi ya Mtendaji Kata.

Wamesema eneo hilo, ni sehemu ya nyumba walizouziwa  na walikuwa wakitumia kwa ajili ya watoto kucheza, kufanyia mazoezi na shughuli za kijamii zenye mikusanyiko ya watu wengi.

Wakati askari hao wastaafu wakitoa malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomary Satura, amekiri ujenzi huo wa Ofisi ya Kata kufanyika na kueleza kuwa maeneo yote ya wazi ni mali ya serikali, hivyo hakuna kosa lililofanyika katika hilo.

Wazee nyumba za bandari Kurasini walalamikia eneo lao la wazi kumegwa
Satura, akiongea kwa njia ya simu na  amesema ni jambo la ajabu kwa wanaolalamika, kwani kinachofanywa ni kuwasogezea wananchi ofisi ya umma karibu, baada ya ile ya awali iliyokuwa Mtaa wa Shimo la Udongo, kutakiwa kubomolewa, baada ya mwekezaji kununua  eneo hilo kwa ajili ya kupafanya bandari kavu.

“Sheria ya ardhi inaeleza kuwa maeneo yote ya wazi ni mali ya serikali, sasa serikali kulitumia eneo lake kwa ajili ya huduma zingine za kijamii kwa nini wengine wahoji, nilidhani wangefurahi tumewasogezea huduma karibu na badala yake wanapinga, hii ajabu kwa kweli,” amesema Satura.

Wakitoa malalamiko yao kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa wakazi hao, Daniel Minde, amesema nyumba hizo walizokuwa wakiishi askari wa Mamlaka ya bandari (Auxiliary Police), ilipofika mwaka 2004  waliuziwa ikiwa ni pamoja na  eneo hilo la wazi lilikuwa likitumika kwa ajili ya parade ambalo hata kwenye ramani yao linasoma.

“Sasa kama ni sehemu ya eneo tulilouziwa, kwa nini leo watu wanaingia na kujenga ofisi na hakuna chochote tulichoambiwa, anataka tukafanyie wapi mazoezi au watoto wetu wakachezee wapi, hii sio haki,”amehoji Minde,

Christina Mwamakula amesema,  sio mara ya kwanza eneo hilo kutaka kuvamiwa kwani tangu mwaka 2021 kumekuwa kukifanyika shughuli mbalimbali, lakini wakawa wanapambana.

Shughuli hizo, amesema ni pamoja na kulazwa magari, kugeuzwa gereji  na wakati mwingine magari makubwa ya mizigo kupita katikati ya mtaa huo hadi kulazimika kuweka geti kwa kuwa yalikuwa yakisababisha nyumba kupata ufa, kutokana na uzito wa mkubwa wa magari.

Pamoja na kupambania huko, amesema Machi 4, 2025 walishangaa kuona matofali, kokoto  na mchanga vikishushwa eneo hilo na siku iliyofuata ujenzi ukawa umeanza wakiambiwa ni Ofisi za Kata zinahamishiwa hapo kutoka zilipokuwa awali mtaa wa Kurasini, Shimo la Udongo.

Romanus Malobola, amesema nyumba walizouziwa zipo 93, hivyo ukichukulia kila familia ina watoto  nane kuna watu zaidi ya 750.

“Idadi hii ya watu, hatuna eneo la kufanyia michezo , hatuna  eneo ikitokea janga tutajikusanya hii ni hatari sana kwa usalama wetu na mazoezi sisi wazee hatuna hela ya kwenda kulipia gym,” amesema Malobola.

Aidha alihoji kwa nini Manispaa hela waliyolipwa kama fidia, baada ya mwekezaji kununua eneo la ofisi ya Shimo la Udongo wasingetafuta eneo jingine hadi waje wavamie hilo lao la wazi.

Akijibu hilo, Mkurugenzi amesema hakuna hela waliyolipwa taslimu na mwekezaji isipokuwa makubaliano ilikuwa ni kuwajengea ofisi nyingine ya kisasa na ndicho kinachofanyika katika eneo linalolalamikiwa na ikishakamilika itakabidhiwa kwao.

Hata hivyo amesema malalamiko kwamba walikuwa wakilitumia kama sehemu ya watoto kuchezea na watu wazima  kufanyia mazoezi hayana ukweli wowote, kwani eneo lote lilikuwa limejaa vibanda vya wakazi hao ambavyo vingine walikuwa wakivifanya maduka.