NBC yajipanga kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa namba moja Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:46 AM Feb 03 2025
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa benki ya NBC, Joseph Lyuba (kushoto) akikabidhi kadi ya gari kwa Darius Kweka, mfanyabiashara mdogo ‘Machinga’ kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa benki ya NBC, Joseph Lyuba (kushoto) akikabidhi kadi ya gari kwa Darius Kweka, mfanyabiashara mdogo ‘Machinga’ kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

WAKATI kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia ya Soka na Takwimu (IFFHS), Ligi Kuu Bara kwa sasa ikishika nafasi ya nne kwa ubora barani Afrika, Wadhamini Wakuu wa ligi hiyo, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), wamesema licha ya mafanikio hayo makubwa yanayoendelea kushuhudiwa bado dhamira ya benki hiyo ni kuhakikisha ligi hiyo inashika nafasi ya kwanza kwa ubora barani Afrika.

Dhamira ya benki hiyo iliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa benki hiyo, Joseph Lyuba, wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha rasmi kampeni yake yenye falsafa ya kimichezo ya ‘Shinda mechi zako Kinamna yako’ ambapo ilikabidhi  zawadi ya gari aina ya BMW X1 kwa Galus Peter Casto maruufu “Kweka”, mfanyabiashara mdogo ‘Machinga’ kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam alieibuka mshindi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye tawi la benki hiyo Kariakoo, Lyuba alisema pamoja na kujivunia mafanikio ya ligi hiyo, benki hiyo ipo kwenye mkakati zaidi kuhakikisha kwamba inashirikiana na wadau zaidi ili kuongeza nguvu kwenye ligi hiyo lengo likiwa ni kuongeza hadhi ya ligi hiyo hadi kufikia nafasi ya kwanza barani Afrika.

“Mafanikio haya yanachochewa na ushirikiano mkubwa baina yetu kama wadhamini wakuu na wadau wenzetu wakiwamo Azam TV, wadau wote wa habari na mashabiki tukiongozwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF). Tunaamini mafanikio haya yatavutia wadau wengi zaidi na kwa pamoja tunakwenda kuifanya ligi hii kuwa namba moja barani Afrika,’’ alisema.

Akizungumzia kampeni ya ‘Shinda mechi zako Kinamna yako’, Lyuba alisema ililenga kuchochea ukuaji wa uchumi miongoni mwa wateja wao kupitia uwekaji wa akiba.

“Tangu kuzinduliwa kwa kampeni hii inayotumia falsafa ya michezo kuboresha maisha ya wateja wetu Aprili mwaka jana, tumeweza kutoa zawadi za gari mbili aina BMW X1 kwa washindi wakuu pia tulitoa fursa kwa wateja hao kujishindia zawadi mbalimbali ikiwamo fedha taslimu, simu za mikononi, ‘laptops’, friji, ‘tablets’ za watoto, bima za afya pamoja na majiko ya kisasa ya kupikia," alisema.

Kwa mujibu wa Lyuba jumla ya zawadi zenye thamani ya Sh. milioni 200 zimetolewa kwa washindi mbalimbali wa kampeni hiyo tangu kuanzishwa kwake.

“Zaidi  ya aina nane ya zawadi zilizotolewa kupitia kampeni hii zilikuwa zipo kimkakati zaidi tukilenga ziwasaidie wateja wetu kwenye kufanikisha majukumu yao kiuchumi ambayo ndio maana halisi ya ‘Shinda mechi zako’ zikiwamo nyenzo za biashara na vitendea kazi vitakavyoweza kuwarahisishia kazi zao,’’ aliongeza.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo, Meneja Masoko wa Benki hiyo, Alina Kimaryo, alisema ilihusisha wateja wote waliokidhi vigezo na masharti na wanaohudumiwa na benki hiyo kupitia huduma zake mbalimbali zikiwamo akaunti za Chanua, Akaunti ya Malengo, Akaunti ya Mwalimu pamoja na akaunti ya Johari.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi yake, Kweka aliyeambatana na mke wake, Miriamu Kweka, pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa makabidhiano hayo alisema ushindi huo umetokana na yeye kujiwekea akiba kupitia akaunti ya malengo kwa ajili ya ada za watoto wake lengo ambalo alifanikiwa kulitimiza.

“Nashukuru pamoja na kufanikiwa kulipa ada za watoto wangu kupitia akaunti ya malengo pia nimefanikiwa kupata zawadi ya gari litakalonisaidia kuwafikia zaidi wateja wangu huko mitaani. Nashukuru kwa kuwa zawadi hii itanirahisishia ‘Kushinda mechi zangu’’, alisema Kweka.