TUNAPOZUNGUMZIA kuhusu kaya maskini, tunagusa zile zenye umaskini wa kukithiri.
Ni lile kundi ambalo wanakwama kumudu matumizi ya milo mitatu kwa siku ikibaki kuwa bidhaa adimu kwao. Wao ni wa mlo mmoja kwa siku, tena unaopatikana kwa shida.
Nasema, kaya hizo zinakwama hata kuwapeleka watoto wao kliniki au shule. Uwezo wa kufanya hivyo nao unabaki kuwa bidhaa adimu.
Mavazi yakiwa ni lingine nyeti, ikiwamo hata katika orodha kitaifa kuhusu hadhi ya binadamu, kwa kaya hizo nguo za kuvaa ni changamoto, huku makazi wanayoishi nayo ni changamoto inayojitegemea.
Pamoja na kaya hizo kupitia magumu na mitihani hiyo, daima serikali yao imesimama katika ajenda ya kutowasahau watu wake. Serikali imeandaa utaratibu wa kuibuliwa kwa kaya hizo na kuziingiza katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, akasema kuwa zaidi ya kaya milioni moja nchini Tanzania zitanufaika na mpango wa serikali wa kusaidia kaya zisizojiweza, ili ziweze kupata huduma stahiki za afya kupitia sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Mhagama anayasema hayo jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Ameyasema hayo katika kikao na Kamati ya Bunge ya Huduma ya Afya na Masuala ya Ukimwi, chombo hicho kikiongozwa na Mwenyekiti Elibariki Kingu.
Akatamka: "Tanzania bara inajumla ya kaya milioni14.8 ambapo kaya milioni 3.9 ni kaya zisizo na uwezo."
Waziri huyo wa Afya, akaendelea kusema kuwa kuna kaya milioni 1.2, ambazo ni sawa na asilimia 32.3, serikali ikiwa imejipanga kuanza kugharamia Bima ya Afya kwa Wote kwa kundi hilo.
Anasema, kundi hilo litatambuliwa kama kaya zenye umaskini uliokithiri, zinazotambuliwa na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) unaohusika na kunusuru kaya masikini.
" Kifungu cha 25 Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura Namba 161, kimeanzisha mfuko wa kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo, ambao serikali imejipanga kuanza ugharamiaji wa Bima ya Afya kwa Wote,” anatamka waziri.
Anasema kuna jumla ya kaya milioni 1.2 ambazo zimetambuliwa kuwa na kaya zenye umaskini uliokithiri.
Anaongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya, imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikijumuisha watoa huduma za afya na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya.
Hapo kunalengwa kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unafanikishwa kwa ufanisi, hivyo matarajio ni wananchi wasio na uwezo watanufaika na huduma hizo.
Waziri ana maoni kwamba wizara yake inazidi kuimarisha ubora wa huduma za afya katika vituo vya utoaji huduma hizo, akiwa ana uchambuzi wa namna hii:
Anatumia kauli: " Miundombinu inaboreshwa, upatikaji wa dawa vifaa tibà na vitendanishi ikiwamo uendelezwaji wa wataalamu na ubingwa bobezi."
Anaongeza kuwapo uimarishwaji kada mpya za tiba, pamoja na huduma za uzazi wa dharura na watoto wachanga (EMONC) katika ngazi ya msingi.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. Irene Isaka, anasema wamejipanga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama, kwa kusimamia utekelezaji wa miongozo ya tiba.
Hapo kuna kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mtindo bora wa maisha, lengo ni kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED