SERIKALI inatarajia kuandikisha watoto zaidi ya milioni 1.8 wa elimu ya awali na wengine milioni 1.7 watakaoanza darasa la kwanza mwaka ujao wa 2025. Kutokana na hilo, kinachoendelea ni kuhimiza wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wao.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anawaagiza wazazi na walezi kutimiza wajibu wa kuwaandikisha watoto wao wote wenye umri wa kwenda shule badala ya kuwaacha wakauze maandazi, karanga na miwa mitaani.
Ninaamini uandikishaji wa sasa hauna lawama kama ilivyokuwa zamani ambapo baadhi ya wazazi na walezi walikuwa wakiwalaumu walimu wakuu kuwa wanatoza fedha za madawati wakati wa kuandikisha.
Baadhi ya wazazi na walezi huwa wanalalamika wakidai kuwa wanaombwa fedha, kwa ajili ya kununua madawati na kusababisha wasio nazo kushindwa kuwaandikisha watoto wao.
Akiwa katika ziara mkoani Simiyu Waziri Mkuu anawapa jukumu watendaji wa kata wote wakae na watendaji wa vijiji na mitaa kuwahimiza uandikishwaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule, kwa kuwa kila mtoto wa Kitanzania anatakiwa kuwa shule.
Katika ufafanuzi wake anasema mtoto wa Kitanzania anatakiwa kwenda shule, kwa kuwa ameandaliwa utaratibu wa kupata elimu kuanzia chekechea, shule za msingi hadi sekondari.
Kwa maelekezo hayo ya serikali, ni vyema wazazi na walezi nao wakauzingatia kwa manufaa ya baadaye ya watoto wao badala ya kuwafanyisha kazi wakiwa hawajafikia umri wa kuingia katika ajira.
Ikumbukwe amewekeza kwenye upatikanaji wa elimu, kwa kutoa fedha ya ujenzi wa shule, madarasa na mabweni, lakini pia inatoa elimu bure, ili kila mtoto wa Kitanzania apate fursa ya kusoma.
Kwa unafuu huo, ninadhani kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kuhakikisha mtoto wake anapata elimu kwa kumnunulia mahitaji yote ya shule, kwani mzigo mwingine unabebwa na serikali.
Itakuwa ni jambo la kushangaza iwapo bado kutakuwa na baadhi ya watu ambao watashindwa kuwaandikisha watoto wao ili waanze elimu ya awali au msingi wakati elimu ikitolewa bure.
Hadi Waziri Mkuu kuwahimiza kuandikisha watoto, maana yake ni kwamba bado wapo wale ambao hawajaona umuhimu wa elimu. Watu wa aina hiyo wangesaidiwa kujua kuwa elimu ina manufaa makubwa.
Elimu ni zaidi ya kusoma, kuandika na kuhesabu, ni moja ya uwekezaji muhimu ambao nchi inaweza kufanya, husaidia watu kufanya kazi vizuri na inaweza kuunda fursa za ukuaji endelevu wa uchumi kwa siku zijazo.
Vilevile, elimu pia inawapa watu ujuzi muhimu na zana za kuwasaidia kujikimu wao wenyewe na watoto wao. Pia inasaidia kuwa na uwezo wa kujitegemea kifedha, lakini si hilo tu, pia inakufanya uwe na hekima zaidi ili uweze kufanya na kuchukua maamuzi binafsi.
Aidha, elimu huathiri zaidi uelewa wa watu wa tofauti kati ya mema na mabaya. Mtu aliyeelimika anafahamu vyema madhara ya matendo haramu lakini asiye na elimu ana uwezekano mdogo wa kushawishiwa kufanya jambo ambalo si sahihi au sahihi.
Maana yake ni kwamba, ikiwa umeelimishwa, unafahamu vyema haki zako, sheria na wajibu kwa ajili ya kuboresha jamii. Hivyo, elimu ni muhimu kwani pia huchangia katika maelewano ya kijamii na amani.
Lakini pia dunia inabadilika kila kukicha huku teknolojia mpya ikizidi kuibuliwa, hivyo bila elimu ni vigumu watoto kwenda na mabadiliko, lakini aliyeelimika itakuwa rahisi kwake kufahamu vizuri teknolojia.
Kwa mantiki hiyo wazazi na walezi wasibaki nyuma kwa kuwapa watoto vitu vidogo vidogo vya kuuza badala ya kuwaandikisha wakapate elimu ya kuwawezesha kupata elimu ya kuwasaidia katika maisha ya baadaye.
Pamoja na hayo, waandikishaji waepuke kurushiwa lawama ambazo hujitokeza kuwa huwatoza fedha wazazi na walezi wanapokwenda kuandikisha watoto wao na kufanya wengine washindwe kuwaandikisha.
Baadhi ya wazazi na walezi huwa wanalalamika wakidai kuwa wanaombwa fedha kwa ajili ya kununua madawati na kusababisha wasio nazo kushindwa kuwaandikisha watoto wao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED