KESHO Wakristo wote duniani wanaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa mwokozi wao Yesu Kristo.
Kumbukumbu hii ni muhimu kwa sababu duniani kote wanaadhimisha kwa kuanza kupamba mapema sehemu mbalimbali, iwe kwenye maduka makubwa, ofisi, sehemu za starehe barabarani ili kuashiria kuwa sikukuu hiyo imewadia.
Wanaojua umuhimu wa sikukuu hiyo huitumia kutoa zawadi kwa marafiki, ndugu na jamaa na makundi yasiyojiweza ili kuonesha ishara ya upendo.
Kwenye maduka mbalimbali bidhaa nyingi hupunguzwa bei ili kumwezesha kila mtu kumudu kununua mahitaji na kuweza kufurahia sikukuu hiyo kwa shangwe.
Kwa wafanyabiashara wanaofanya hivyo ni kuonesha kuwa wanawajali wateja wao na vilevile hupata baraka katika biashara zao na kuongeza mapato.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wafanyabiashara hutumia kipindi hiki kujinufaisha zaidi badala ya kuwajali wateja wao.
Kipindi hiki hutumika kupandisha bidhaa bei hasa vyakula na mavazi na kuwaumiza wateja.
Wanafanya hivyo kwa kutambua kuwa lazima watu watanunua kwa sababu wapo katika uhitaji. Hiki ni kipindi ambacho wazazi wengi huingia kwenye mawazo kutokana na familia kutaka kununuliwa nguo mpya na vile vile kula chakula kizuri.
Wafanyabiashara hutumia mwanya huo kuhakikisha kuwa huo ndio muda wa mavuno kwao. Kwa mfano nguo iliyokuwa ikiuzwa Sh. 20,000 itapanda na kuwa Sh. 25,000 hadi 30,000.
Kwa upande wa chakula, kipimo cha sado moja ya nyanya ambayo ilikuwa inanunuliwa kwa Sh. 2,500 itapanda hadi Sh. 4,000.
Kilo moja ya nyama ambayo ilikuwa inanunuliwa kwa Sh. 8,000, sasa itapanda hadi Sh. 12,000.
Huu sio uungwana hata kidogo, kila mmoja anapenda siku kama hiyo kukaa na familia yake ale chakula nao chakula kizuri, lakini kwa ubinafsi wa kupenda fedha za haraka, mnawaumiza wenzenu.
Ni vigezo vipi vinavyosababisha bidhaa hizo kupanda ghafla wakati wa sikukuu na inapomalizika, bei zinarudi kama kawaida.
Ukiwauliza wafanyabiashara wanajibu kuwa eti gharama za usafirishaji kipindi cha sikukuu zinapanda. Zinapanda vipi wakati bei za dizeli na petroli ziko palepale, wakati bei hizo ndio huchukuliwa kama sababu ya kupanda kwa gharama.
Wafanyabiashara kueni na huruma na wenzenu, kumbukeni kuwa kipindi hiki ndicho cha kujitafutia thawabu kwa Mwenyezi Mungu.
Katika sikukuu hizi za mwisho wa mwaka kuna mambo mengi yanayojitokeza, hivyo ni lazima jamii iwe makini kulinda familia zao.
Watoto hupendelea kwenda fukwe za bahari kusherehekea, ni vizuri kuwa na uangalizi wa watu wazima ili kuepuka majanga.
Vile vile, kuna watu wanaosubiri familia zitoke kwenye nyumba zao halafu wao watumie muda huo kufanya uovu wa kuvunja nyumba hizo na kuiba mali. Jamii lazima iwe makini ihakikishe familia inapotoka inaacha mtu wa kuangalia.
Hiki sio kipindi cha kusherehekea kwa kufanya vurugu. Ni kipindi cha kufurahi kwa amani na kumshukuru Mungu kwa kuweza kukulinda mwaka mzima na kuiona tena siku hii.
Kuna wengine walitamani kufurahi katika siku hiyo, lakini sasa hivi ni wagonjwa wako vitandani wakipigania maisha.
Basi kwa waliobahatika kuwa salama ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa kutoa sadaka ili uendelee kubarikiwa.
Tunawatakiwa wote maandalizi mema ya Krismasi na Mwaka Mpya 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED