UCHAFUZI wa mazingira umeleta athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi, hali iliyosababisha baadhi ya maeneo kukosa mvua na kuleta upungufu wa mvua.
Athari za mabadiliko ya tabianchi zimeshuhudiwa katika baadhi ya maeneo ambako mvua imenyesha kupita kiwango na watu kukosa makazi na hata kusababisha vifo.
Umuhimu wa kuhifadhi mazingira unatakiwa uanzie katika ngazi ya familia na kupanua wigo hadi kwa wadau mbalimbali.
Watu muhimu na wanaosikilizwa katika jamii ni viongozi wa dini ambao Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahi kusema kuwa wanayo nafasi kubwa na kuwataka iwe ajenda maalum katika ofisi za umma, za binafsi au kwenye taasisi.
Umuhimu wa jamii kushiriki katika uhifadhi mazingira ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Aidha, jitihada ambazo Rais Samia amezichukua ili kuhakikisha suala la nishati safi linakubalika ni kukataa kukata miti na kuhamasisha kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Rais Samia amekuwa kinara wa nishati na alienda nchini Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, jambo ambalo ni ni fahari kwa nchi ya Tanzania.
Wajasiriamali wamepewa fursa kuanzisha biashara ya kuuza mitungi na majiko ya gesi hadi kwenye ngazi ya vijiji ili nishati hiyo iweze kupatikana kwa urahisi hali ambayo itaweka ukomo wa matumizi ya mkaa na kuni nchini.
Pia, serikali imechukua hatua za kisera na kimkakati ili kuleta matokeo chanya zikiwamo za kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021; Kutungwa kwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014; kuandaa na kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032; kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2021 hadi 2026; na kutungwa kwa Kanuni na Miongozo inayohusu masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.
Wizara inayosimamia mazingira imetakiwa ishirikiane kwa karibu na wizara za kisekta kuhakikisha maadhimisho mbalimbali ya kitaifa yanayogusa masuala ya mazingira yanatumika kikamilifu kuwezesha jamii kupata uelewa na kuweka alama za kudumu na matokeo yanayopimika kuhusu utunzaji mazingira ikiwamo Siku ya Upandaji Miti, Siku ya Hali ya Hewa, Siku ya Maji, Siku ya Ardhi Oevu, Siku ya Mazingira na Siku ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni.
Uhamasishaji kuhusu utunzaji wa mazingira, Waziri Mkuu amezitaka ofisi za mikoa na wilaya, zisimamie suala hilo na kusisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za mazingira na ikibidi watumie mitandao ya kijamii kusambaza elimu hiyo.
Hiyo itasaidia kuongezeka kwa ufahamu miongoni mwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kutasaidia kupunguza uharibifu na kuimarisha usimamizi wa mazingira. Aidha, elimu ijumuishe matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira ikiwamo matumizi bora ya ardhi, maji na nishati ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinabaki kuwa za kudumu kwa vizazi vijavyo.
Utunzaji wa mazingira unaanzia nyumbani kwako, sehemu yako unayofanyia shughuli za kukuingizia kipato na hata barabarani unapopita.
Kila mmoja anapoona mwenzake akiharibu mazingira ana jukumu la kumkemea ili ajue kuwa anachokifanya kinaathiri jamii na taifa kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED