KARIBU kila sehemu wananchi wanaendelea kuhamasishwa kuchangia ujenzi wa miradi hasa majengo kwa ajili ya maabara za sekondari za kata.
Hayo yanafanyika, kwa sababu kila sekondari ya kata inapaswa kuwa na maabara tatu kwa masomo ya fizikia, kemia na bailojia ambazo ujenzi wake unajengwa kwa kushirikisha nguvu ya serikali na wananchi.
Pamoja na hayo, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo kama hazitafanyiwa kazi haraka, huenda zikakwamisha juhudi zinazolenga kuhakikisha kila sekondari ya kata inakuwa na maabara tatu.
Miongoni mwa changamoto hizo ni baadhi ya shule kuwa na majengo na maabara zenyewe, lakini hazina wataalamu wa maabara hizo (Laboratory Technician), kwa ajili ya kuziendesha.
Uhaba huo wa wataalamu wa maabara, unaweza kurudisha nyuma jitihada za mafunzo kwa vitendo katika shule za sekondari licha ya kwamba kuna maabara katika shule hizo.
Ninaamini walimu wa masomo ya sayansi hawawezi kuwa na uwezo wa kutumia maabara kikamilifu, badala yake wataalamu wake ndio ambao wanahitajika ili wafundishe wanafunzi kwa ufasaha.
Wapo baadhi ya wanafunzi waliowahi kukaririwa na vyombo vya habari wakisema ukosefu wa wataalamu wa maabara katika shule zao unasababisha walimu wa masomo ya sayansi wageuke kuwa wataalamu wa maabara hizo, na kwamba hawana ujuzi wa kutosha wa kuzitumia.
Kwa kuwa katika kuboresha elimu jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali, ikiwamo ujenzi wa madarasa, majengo ya maabara, ununuaji wa madawati na mahitaji mengine ya muhimu shuleni, ninadhani hata hili la wataalamu wa maabara lingepewa uzito zaidi.
Ninadhani ipo haja walimu wa masomo ya sayansi kupewa mafunzo ya jinsi ya kutumia maabara hizo ili waweze kufundisha wanafunzi, wakati serikali ikijiandaa kuweka wataalamu hao kila sekondari.
Wapo walimu ambao wanatajwa kutumia maabara hizo kufundisha wanafunzi. Ninadhani ndio wangepewa kipaumbele cha kufundishwa jinsi ya kutumia maabara hizo ili wasaidie wanafunzi.
Kama mwalimu anajaribu kufundisha kwa kutumia maabara hizo, maana yake ni kwamba ana uelewa nazo, hivyo akiongezewa ujuzi inaweza kuwa rahisi kwake kutumia kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi.
Hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza tatizo lililopo la ukosefu wa wataalamu hao ambalo linasababisha wanafunzi wasijifunze masomo ya sayansi kwa vitendo kama inavyotakiwa.
Iwapo walimu wataongezewa mafunzo ya utaalamu wa maabara wakijikita zaidi kwenye vitendo, watakuwa wamesaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa wataalamu hao katika sekondari mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa mwalimu anapohitimu mafunzo ya ualimu kama ni wa masomo ya sayansi, mara nyingi anakuwa anajua kufundisha kwa nadharia, hivyo hawezi kuwasaidia zaidi mwanafunzi kwa vitendo.
Lakini kwa kuwa ana uelewa wa kutumia maabara hizo, ninaamini akifundisha jinsi ya kuzitumia anaweza kuelewa kirahisi na hivyo kuwafundisha wanafunzi wake kwa vitendo
Kuendelea kuwapo kwa sekondari ambazo hazina wataalamu hao, kunaweza kukwamisha serikali katika mipango yake ya kuandaa wataalam wa fani mbalimbali wa baadaye.
Vilevile, kuwapo kwa wataalam hao shuleni kunasaidia wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kirahisi kwani watakuwa wanafanya kwa vitendo kuliko ilivyo sasa wanapojifunza kwa nadharia.
Ni muhimu kutambua kuwa kutumia walimu wasio na ujuzi katika maabara msaada wao kwa wanafunzi si mkubwa, hatua za haraka zinahitajika kufanikisha azma ya kuwa na mafanikio katika elimu kwa vitendo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED