LILIKUWA ni jambo la kushangaza, kuhuzunisha na kuchekesha kwa wakati mmoja pale mwamuzi Omri Mdoe alipoonekana kumsukuma mchezaji Yusuph Dunia katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya Mashujaa na Simba, uliochezwa Ijumaa iliyopita katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Mdoe alionekana kufanya tukio hilo akiwa katika harakati za kumtuliza Dunia aliyeonekana kulalamika kwa kutokukubaliana naye, alipoamuru faulo ilekezwe kwao baada ya Joshua Mutale kufanyiwa madhambi.
Mdoe alifanya hivyo mara mbili na baadaye wachezaji wa Mashujaa wakaja kumuondoa mwenzao.
Mmoja wa watu walio kwenye Kamati ya Waamuzi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu haruhusiwi kuliongelea suala hilo kimaadili, amesema kamati hiyo inaweza kufanya kazi ya kupitia tukio hilo na kuona kama alifanya sahihi au la.
Ni tukio ambalo limezua gumzo kubwa sana kwa mashabiki na hasa kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakitengeneza vibonzo.
Ukiangalia kwenye mchezo huo utagundua mwamuzi huyo aliogopa kutoa kadi si kwenye tukio hilo tu bali kwenye mchezo mzima ambao ulitawaliwa na matumizi ya nguvu wakati mwingine kupita kiasi.
Cha ajabu ni kwamba kulikuwa na kadi moja tu ya njano kwenye mchezo huo licha ya kwamba takwimu zilionesha idadi kubwa ya madhambi.
Hata Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alilalamika juu ya wachezaji wake kuchezewa vibaya, lakini mwamuzi hakuchukua hatua stahiki.
Ndiyo maana haikushangaza kuona alishindwa kumuonesha mchezaji kadi badala yake akaamua kumsukuma naye. Ina maana Mdoe hajui kuwa kadi ndiyo silaha yake uwanjani na si mdomo, mikono au ukali? Hapa inashangaza kweli.
Hii inaonyesha kuwa ni mmoja wa waamuzi ambao hawajiamini, au aliamua tu kuwa mechi hiyo asioneshe kadi nyingi za njano kwa sababu anazozijua yeye.
Kwa waamuzi wanaojua kazi zao na wanaojiamini, wakati mchezaji anakuja angepeleka tu mkono kwenye mfuko wa chini kuonesha kama anatoa kadi nyekundu, sidhani mchezaji yule angefika hadi pale alipo.
Nitoe pongezi kwa mwamuzi Ahmed Arajiga na wasaidizi wake waliochezesha mchezo kati ya Yanga na Azam FC, na waliochezesha mchezo kati ya Singida Black Stars na Yanga pale Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, kwani walionekana kuchezesha kwa mamlaka, huku wakiwadhibu kwa kadi kila kosa lililoonekana linastahili kufanya hivyo.
Wakakati mwingine wachezaji ni kama wanafunzi tu au watoto, hufanya jinsi ambavyo anayewaogoza alivyo.
Kama ni dhaifu basi wanaweza kumpelekesha, lakini akiwa mkali wanatii shuruti, na ndiyo ilivyokuwa.
Na mara nyingi mwamuzi anayeamua tukio kwa usahihi huwa hana kazi kubwa ya 'kubalansi' mchezo kwani huacha mchezo ujiendeshe wenyewe, anachofanya yeye ni kuamua matukio kwa jinsi yanavyojitokeza tu.
Wale wa 'kubalansi' inafika wakati mechi inawashinda kwa sababu mwanzo aliacha huku, linatokea jambo lingine kubwa upande mwingine anashindwa kufanya maamuzi kwa sababu awali aliacha upande mwingine.
Kamati ya Waamuzi, Chama cha Waamuzi nchini, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na Bodi ya Ligi (TPLB), inadibi kufanya uchunguzi kama baadhi ya waamuzi wanafanya hivi kwa shinikizo kutoka mahali fulani, uwezo mdogo, presha ya mchezo, malipo madogo, wanacheleweshewa posho zao au kuna nini?
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED